Na Mwandishi Wetu, Pemba
Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa na uwezo mdogo wa kisiasa walionao viongozi wa ACT Wazalendo Zanzibar , tokea kilipompoteza aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho , Marehemu Maalim Seif Sharrif Hamad.
Vile vile, CCM imekitaja ACT kimepungukiwa na viongozi mahiri, wenye uwezo mpana kisiasa na waliobaki sasa ni wapiga porojo majukwaani ndio maana hawana Sera wala Ilani inayowaongoza kwenye uchaguzi mkuu 29 Oktoba 2025.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema kwa hilo anawapa pole ACT kwa sasa kwani kinaongozwa kiujanja ujanja.
"Hivi sasa chama hicho kinaongozwa na wanasiasa magube na makanjanja" alidai Mbeto.
Mwenezi huyo alisema chama chochote makini cha siasa, hutangaza sera zake, kutaja dira na mwelekeo ili kichaguliwe, badala yake wamebakiwa na viongozi walioshindwa kujenga hoja mbele ya umma.
Alisema baada ya viongozi wa ACT kushindwa kuwa wabunifu katika kuendesha siasa za kisasa, kimebaki kulitumia jina Marehemu Maalim Seif huku kikitegemea kupata ushindi wa Urais.
"ACT kimepoteza sifa baada ya kutokea kifo cha Maalim Seiif. Hivi sasa kinasubiri majaliwa baada ya kukosa matarajio. Hiyo ni shida kwa chama kutegemea uwezo wa mtu mmoja kukipa chama uhai wa kisiasa "alisema.
Alibainisha kuwa chama cha siasa lazima kiwe na misingi na kitengeneze viongozi na sio kuokoteza.
Mbeto alisema chama chao huandaa viongozi toka Chipukizi, Umoja wa Vijana (UVCCM ) na baadae CCM na ndio maana kina hazina kubwa ya viongozi wenye sifa za kuwatumikia wananchi.
"Ndio maana hata kikifanya mabadiliko ya viongozi hakipati athari zozote tofauti na ACT au vyama vingine vya upinzani" alisema.
Mbeto ambaye ametaka waZanzibari kumchagua Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa Rais Zanzibar ili amalizie miradi ya maendeleo aliyoianza, alisema kuwa ACT kimepoteza idadi kubwa ya wanasiasa madhubuti ambao walifukuzwa CCM na kuhamia CUF enzi hizo.
Wanasiasa hao ambao baadae wakawa ACT ambako wamekutana na kadhia za kiuongozi na kupoteza dira.
"Huko wamekutana na adha na karaha ya mtu anayeitwa Ismail Jussa Ladhu matokeo yake wakaletewa figisu chaguzi za ndani ikiwa ni pamoja na ya Urais na matokeo yake ndio yanayoonekana hivi sasa" alisema mwenezi huyo.
Alibainisha kuwa 1987 kundi la wanasiasa hodari waliotimliwa CCM na kujiunga CUF miongoni mwao waliandaliwa wakiwa CCM na kukomaa kisiasa.
"Kwa Siasa za uzushi na fitna za Ismail Jussa Ladhu, marehemu Maalim Seif Sharriff akafitinishwa na Hamad Rashid Mohamed na upande mwingine Mohamed Dedes na Juma Duni ili mmojawapo asigombee Urais " alisema Mbeto .
Kutokana na hali hiyo ndio maana chama hicho kimepotea na huenda kikasambaratika baada ya 29 Oktoba 2025.

0 Comments