Na Mwandishi Wetu, Kibamba
Mgombea Ubunge Jimbo la Kibamba kwa tiketi ya CCM Angellah Kairuki amewaomba wakazi wa Kibwegere kumpa kura nyingi ili awe mbunge wao na kusaidiana nao kukabili changamoto zinazokabili jimbo hilo na wakazi wake.
Akizungumza mara baaďa ya kupokea changamoto za makundi mbalimbali katika ukumbi wa Mashingo, Kibwegere Kairuki alisema kuwa Kibamba anaijua na changamoto zake hivyo yupo tayari kushirikiana na wakazi hao kuzikabili ili kuleta maendeleo jimboni humo.
Alisema anajua mahitaji ya vivuko kuunganisha maeneo ya Jimbo hilo na changamoto ya ajira kwa vijana na kumtaka Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Humphrey Mtili kumuandalia orodha ya vijana wasio na ajira rasmi na wasifu wao ili pindi akipata ridhaa ya wanaKibamba kuwatumikia bungeni aweze kulishughulikia.
"Kuna vijana wahitimu wa vyuo vikuu wapo wengine wamemaliza na kuna wanaosubiri matokeo nipate orodha yao kwani zipo schoolership za masomo nje ya nchi tunaweza kusaidiana kuzipata" alisema.
Mgombea huyo aliahidi ahidi kuipigania barabara ya Kibamba-Mpiji ili kilometa zaidi ya tano zilizobaki kumaliziwa haraka ili kuchochea maendeleo ya Kibwegere na Kibamba kwa ujumla.
Kairuki ambaye amesisitiza amani kuelekea na baada ya uchaguzi amewataka kuzitumia fursa zilizoletwa na serikali ya CCM chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jimboni humo ikiwa ni pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kinachojengwa jirani na Shule ya Msingi, Kibwegere.



0 Comments