DKT. MWINYI : TUTAJENGA SHULE ZAIDI ZA GHOROFA

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Wakazi wa Tomondo Uzi na Kinuni katika Mkoa wa Magharibi watapatiwa shule za kisasa za ghorofa zenye mahitaji yote muhimu ya kufundishia kufuatia mkataba wa ujenzi wa shule 29 Unguja na Pemba.

Akizungumza wakati wa mkutano mkubwa wa kampeni, uliofanyika Pangawe 01 Oktoba 2025, mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema kuwa anajua changamoto zinazowakabili hivyo anaomba ridhaa yao ili awatatulie.

Alisema kuwa ameambiwa Tomondo Uzi na Kinuni wanahitaji shule nami nawaahidi kuwa tunakuja kujenga shule, tena za ghorofa sio hizi za kawaida.

" Pia Kijitoupele Mashine ya wanahitaji shule ya maandalizi nayo tunakuja kuijenga" alisema.

Alibainisha kuwa barabara zote za ndani zitajengwa kiwango cha lami na zipo katika mpango wa serikali kinachosubiriwa ni muda tu.

" Kuna kampuni tuna mkataba wa kujenga barabara zote za ndani Unguja na Pemba, suala ni muda tu mkandarasi anakuja" alisema Dkt. Mwinyi.

Alisema Kwalala Kidutani wanaenda kupata kituo cha afya kama walivyo omba.

Mbali ya mradi wa viwanja 17 vya kisasa vya michezo kila wilaya, miradi hiyo ikikamilika, alisema Dkt. Mwinyi, vitajengwa vingine vya mazoezi kila jimbo ili kuibua vipaji kwa vijana.

Suala la ajira kwa vijana ndio sera mama ya CCM na atahakikisha, wanapata ajira kwa wingi kadiri inavyowezekana.

Ajira hizo ni kuanzia serikalini, katika viwanda vinavyoanzishwa na wawekezaji na kupitia mikopo ya biashara isiyo na riba.

Katika mkutano huo, Dkt. Mwinyi aliwataka wananchi wa Pangawe kuwapuuza wapinzani kutokana na kukosa sera.

"Sijasikia wanasema lolote kuhusu elimu, afya, miundombinu ya barabara hivyo ni wazi kuwa hawana sera wala uwezo wa kuongoza" alisema mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya CCM.

Post a Comment

0 Comments