TAARIFA KWA UMMA
Chama cha National League for Democracy (NLD) kinapenda kuuarifu umma kuwa Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha NLD, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, leo Agosti 27, 2025 amerejesha rasmi fomu za uteuzi wa kugombea urais katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizopo Njedengwa, Jijini Dodoma.
Mhe. Doyo aliwasili katika ofisi hizo akiambatana na mgombea mwenza wake, Bi. Chausiku Khatibu Mohamed, pamoja na viongozi waandamizi wa chama cha NLD. Fomu zote zilizojazwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria zimewasilishwa kwa mafanikio, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurejesha fomu hizo, Mhe.Doyo alisema. “Leo ni siku ya kihistoria kwa chama chetu na kwa Watanzania kwa ujumla. Tumechukua hatua hii kwa nia njema ya kuleta mabadiliko ya kweli na kulinda haki za kila Mtanzania. Tulichukua fomu na sasa tumerejesha fomu zetu huku tukikidhi vigezo vyote kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.”
Baada ya kupitia na kuhakiki fomu hizo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemteua rasmi Mhe. Doyo Hassan Doyo pamoja na mgombea mwenza wake, Bi. Chausiku Khatibu Mohamed, kuwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha NLD katika uchaguzi wa mwaka huu.
Chama cha NLD kinaendelea kuwa na imani thabiti kwamba Mhe. Doyo ni kiongozi mwenye maono makubwa, uzoefu mpana na dhamira ya dhati ya kulitumikia taifa kwa misingi ya haki, uwazi na uadilifu.
Tunatoa wito kwa wanachama wetu na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kushiriki kikamilifu katika hatua zote za uchaguzi kwa amani, mshikamano, uzalendo, haki, maendeleo.Imetolewa na.
Don Waziri Mnyamani
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Taifa
Chama cha NLD



0 Comments