Katika mazungumzo hayo Mhe. Balozi Matinyi amewasilisha salamu kwa wananchi na Serikali ya Ufalme wa Sweden kutoka kwa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwanadiplomasia namba moja nchini na kusisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza uhusiano wa muda mrefu wa Kidiplomasia na ushirikiano kiuchumi na Sweden.
Vilevile Balozi Matinyi alieleza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ustawi wa uchumi kupitia ushirikiano na Sweden,hususan katika sekta za nishati ,elimu,afya,utafiti mazingira, uzalishaji wa viwandani na miradi ya miundombinu kama vile Reli ya Kisasa (SGR).
Katika mazungumzo hayo,Mhe.Balozi Matinyi alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya Kampuni 101 kutoka Sweden zimewekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwa na thamani ya dola za Marekani Milioni 313.04 na zikichangia ajira takriban 3,877 huku akisisitizia nia ya Tanzania kuimarisha biashara na uwekezaji baina yake na Sweden.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mhe.Stenergard alithibitisha dhamira ya Sweden kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Aidha Waziri Stenergard alihimiza mchango wa Tanzania katika kudumisha amani na usalama duniani hususan katika kusaka suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Ukraine na Urusi.

0 Comments