TABORA.
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya amewataka watumishi wa umma kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, wanapofanya michakato ya ununuzi kupitia Mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na tija.
Ameyasema hayo leo, Aprili 8, 2025 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa taasisi za Serikali kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST.
"Kama ilivyo kwa Mifumo mingine, Mfumo wa NeST ni hatua nyingine muhimu katika kuelekea matumizi bora ya teknolojia katika sekta za umma. Niwasihi tuufanye mfumo huu kuwa sehemu ya kuongeza uwazi, ufanisi katika kazi zenu. Huu Mfumo haupo tu kama suluhisho la mchakato wa ununuzi wa umma bali pia ni njia bora ya kuhakikisha uwazi, ufanisi na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma,” amesema.
Aidha, Dkt. Mboya ameongeza kuwa ili Mfumo wa NeST uweze kutumika vizuri ni lazima kuzingatia sheria na taratibu za ununuzi kwa kuzingatia uadilifu na kuepuka kupindisha sheria hizo.
"Kuna mambo matatu au manne ya kuzingatia. Jambo la kwanza ni lazima kuwa waadilifu katika matumizi ya mfumo kwa kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa katika hatua zote. Sote tunafahamu kuwa ili apatikane mkandarasi au mzabuni ziko taratibu zinazopaswa kufuatwa, sasa ni jambo la msingi kufuata sheria zote na kuepuka kupindisha,” aliongeza Katibu Tawala
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kati na Magharibi PPRA, Mhandisi Suma Atupele amesema, mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Ununuzi na Ugavi kutoka Taasisi nunuzi kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST pamoja na kuwaonesha maboresho yaliyofanyika katika mfumo kwakuwa ujenzi bado unaendelea.
"Katika vipengele vilivyoboreshwa hata vikapelekea tuje tutoe mafunzo haya ni eneo la majadiliano ambayo yanakuwa yamebeba malengo mbalimbali ndani yake. Kipengele cha pili ni upekuzi wa mikataba ndani ya Mfumo wa NeST, na jambo la tatu ni kushughulikia malalamiko na kukata rufaa ndani ya Mfumo,” alibainisha.
Baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru PPRA kwa kuleta mafunzo ambayo wanaamini yataleta mabadiliko katika utendaji kazi wao na taasisi kwa ujumla.
Mafunzo ya kuwajengea watumishi wa Serikali kuhusu Mfumo wa NeST yameanza tarehe 7 – 11 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Mwanakiyungi Mkoani Tabora.
0 Comments