WAAJIRI WATAKIWA KUTHAMINI TAALUMA YA UANDISHI WA HABARI.

Na Mwandishi Wetu.

Wamiliki wa vyombo vya Habari nchini wametakiwa kuithamini Taaluma ya Habari kwa kuwalipa stahili zao na mishahara kwa wakati waandishi wanaofanya kazi katika vyombo hivyo.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Dkt. Egbert Mkoko, tarehe 27 Machi 2025, wakati akizungumza katika kipindi cha Wakeup Call kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha Upendo cha jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mkoko alisema kuwa ni vyema waajiri wakatimiza wajibu wao wa kuwalipa mishahara na stahiki muhimu Waandishi wa Habari kama vile serikali itakavyowapa Ithibati ya kuwatambua kuwa hawa ni Waandishi wa Habari.

"Tunatambua baadhi ya vyombo vya habari vipo hoi katika suala la uchumi kutokana na tathmini iliyofanywa mwaka uliopita ila naamini kupitia bodi ya JAB kuna kitu kitafanyika", alisema Dkt. Mkoko.

Aidha, Dkt. Mkoko alisema kuwa ni vyema Waandishi wa Habari na wamiliki wa vyombo hivyo wakaipa ushirikiano bodi hiyo ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi kwa kuwa imekuja kwa ajili ya kuipa heshima taaluma ya habari.

"Naomba wanahabari mtambue kuwa Bodi hii haikuja kwa ajili ya kuwafungia bali imekuja ili kuipa heshima taaluma ya habari na hivyo iweze kutambulika na kupewa heshima kama taaluma nyingine," alisema Dkt. Mkoko.

Bodi ya Ithibati ya Wanahabari Tanzania imeundwa kwa mujibu wa sheria, lengo kuu ni kukuza taaluma ya waandishi wa habari.

Post a Comment

0 Comments