Na Mwandishi wetu
KIGOMA.
Maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu (Idara ya Menejimenti ya Maafa) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia uhamaji (IOM) wameendesha semina ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya maafa katika jamii.
Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 25 Machi 2025 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo yamehudhuriwa na washiriki 50 ikiwemo Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Mtaa Kamati za Maafa za Kata na Vijiji pamoja na mtaa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Bi.Petronila Gwakila ambaye ni Afisa Mazingira ndani ya Manispaa hiyo amesema, mafunzo hayo yameletwa wakati sahihi ambapo manispaa inatarajiwa kupata mvua ambazo mara nyingi mvua hizo husababisha maafa mbalimbali na kufanya wananchi kutofanya shughuli zao za kila siku za kuwapatia kipato hivyo mafunzo haya yataweza kuleta muamko katika kukabili maafa pindi yatakapotokea.
"Kwa hiyo ndugu zangu tumepata wakufunzi hawa juu ya masuala ya Maafa ningependa sana tuwe makini kusikiliza kutokana na kwamba hili jambo ni muhimu maana si mara moja wala mara mbili maafa hasa ya mafuriko yanatukuta sana katika maeneo yetu hata sasa mvua zimeshaanza na tumeanza kuona athari zake hivyo tusikilize ili tujue namna ambavyo tunaweza kujinusuru na jambo hili” alisema Bi.
kwa Upande wake Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Naibu Kamishina Hamisi Rutengo amesema, lengo la kutunga Sheria ya Maafa ni kuwezesha shughuli za usimamizi wa Maafa kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia ushauri wa kitaalamu na maelekezo ya viongozi ili kupunguza madhara ya majanga.
"Semina kama hizi za kujengeana uwezo zinatukumbusha namna ya kukabiliana kabla ya tukio kutokea, wakati wa tukio kutokea, na baada ya tukio kutokea kwa hiyo tupo hapa kwaajili ya kujenga uwezo huohuo wa sisi mmoja mmoja hadi ngazi ya kitaifa na serikali haikotayari kupoteza watu kwa makusudi na ndio maana tunaleta semina hizi kwenu ili mkienda huko muweze nanyi kutoa elimu kwa wengine ili tupunguze madhara mengi zaidi." alisema Naibu Kamishana Rutengo
Naye, Afisa Miradi Msaidizi kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia uhamaji (IOM) Bw. Reuben Mbugi amesema semina ya upunguzaji wa hatari za maafa ni moja ya shughuli za mradi wa pamoja wa Kigoma unaotekelezwa na mashirikia ya Umoja wa Mataifa lengo ikiwa ni kuhakikisha Serikali inasaidiwa katika kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kabla na baada ya kupata athari za Majanga mbalimbali.
Semina hii inafanyika kwa siku mbili ambapo imeanza leo tarehe 25 Machi hadi tarehe 26 Machi 2025.
0 Comments