RC KUNENGE AWAFUNDA VIONGOZI WA MASHIRIKA YA UMMA


RC Kunenge  akizungumza na Viongozi wa  Mashirika ya Umma kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Uongozi  yaliyoanza tarehe 20 hadi 26 Oktoba,2024.

Kibaha,Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Mashirika ya Umma, Halmshauri na serikali kuu wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata vipaumbele vya Rais kwani wao ndio watekelezaji wa mambo ambayo yanatakiwa kuleta matokeo chanya.

Kunenge ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Uongozi na Menejimenti kwa viongozi wa wa Mashirika ya Umma yanayofanyika katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kwamfipa Kibaha.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuna mambo ambayo anatarajia yatokee kulingana na vipaumbele vyake 
Mashirika ya Umma ndio yanatakiwa kufanya hivyo kwa kujipanga katika utendaji wao.

"Lazima ujue vitu gani utafanya vilete tija, lazima uweke malengo  na kufanya tathmini kutokana na wateja unaowahudumia na hii siyo kwa Mashirika ya Umma pekee hata kwa watumishi wa Serikali kuu lazima ujue unachofanya kinaendana na vipaumbele vya Rais," amesema.

Kunenge amesema kuwa viongozi hao lazima waangalie vipaumbele vya Rais wakati wa kutekeleza majukumu yao.

"Vipaumbele vya Rais vimegusa sekta zote kwa upana wake na vimelenga kuwaletea maendeleo wananchi hivyo lazima wahakikishe vinaendana," amesema Kunenge.

Amesema kuwa pia viongozi hao wapime je wanafikia malengo ya Taasisi na kama kuna changamoto waangalie namna ya kuzitatua ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Shule ya Mwalimu Nyerere Profesa Marcelina Chijoriga amezikumbusha Taasisi hizo pia kujua wateja wao ni akina nani na kuachana na tabia ya kujifungia ndani na kujiaminisha kwamba wanafanya kazi nyingi na badala yake wawe na mabadiliko katika utendaji wao kwa kufanya kazi kuendana mazingira ya kimataifa.

Kunenge pia amesema mashirika hayo yanatakiwa kufanya kazi zao kwa ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na kuwezesha kujiendesha yenyewe  bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu.

Mkuu wa shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Profesa Marcellina Chijoriga amesema ni wakati sasa wa viongozi wa Mashirika ya Umma kuwa na mabadiliko katika utendaji wao sambamba na kuwa wazalendo.

" Tunategemea katika shule yetu kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali na kwa upande wa Taasisi za Umma tunalenga kuwabadilisha viongozi wake kutokana na umuhimu wake wengi mmeona baadhi ya mashirika yamekufa na mengine hayafanyi vizuri," amesema.

Amesema kuwa sasa ni wakati wa kujidhatiti mashirika ya Umma yaweze kufanya kazi kwa uzalendo na ufanisi kukidhi malengo kwa kutoa huduma zinatolewa kwa ufanisi.

Amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwabadilisha viongozi hao wa umma ili walete ufanisi katika utendaji kazi wao.

Chijoriga amesema kuwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma endapo hawatapata mafunzo hawataweza kuboresha utendaji kazi wao hasa ikizingatiwa kuna mambo mbalibali yanabadilika hivyo nao waendane na hali halisi
Wakati huohuo  RC Kunenge amesisitiza  kwa kusema kuwa anawaomba wananchi wa Kibaha na Vitongoji  vya jirani kuwa wastahmilivu katika kipindi hiki cha ukosefu wa usafiri wa magari ya Mwendo kasi ambao umesitishwa kutokana na changamoto  inayowakakabili  UDART  amesema kuwa hali itakapotengemaa usafiri huo  utarejeshwa na tayari serikali imetoa  tamko kuhusiana na kadhia hiyo   lililotolewa na  Waziri Ofiisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohammed Mchengerwa.
Viongozi kutoka katika mashirika mbalimbali wakifuatilia maelekezo yaliyokua yakitolewa na aliyekua mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.

Post a Comment

0 Comments