Onesho hilo lililowashirikisha wasanii nguli wa muziki wa kizazi kipya, Nay wa Mitego, Barnaba, Shilole ‘Shishi Bay’, Kala Jeremiah na mabingwa wa vichekesho hapa nchini, Mkali Wenu na wenzake, hakika lilikuwa la aina yake na liliacha simulizi kubwa kwa mashabiki waliojitokeza kulishuhudia.
Onesho hilo lililoongozwa na DJ Ziro na DJ Max wa Dar Live ambao walizikonga nyoyo za mashabiki, lilianza kwa shamrashamra kwa wasanii waliopanda jukwaani kupiga shoo za utangulizi.
Nusura baadhi ya mashabiki hao wavunjike mbavu kwa vicheko kufuatia vichekesho vilivyoletwa na Mkali Wenu na wenzake kwani jamaa hao ni noma kwa kuvunja mbavu watu, hata walipomaliza kutoa burudani mashabiki waliwaita warudie tena nao wakafanya hivyo.
Ilikuwa kama mvua inataka kutibua onesho hilo lakini mashabiki hawakujali mvua ambayo ilikuwa inanyesha kwani waliendelea kula shangwe bila kujali mvua iliyokuwa inamwagika kwa wingi.
Hata Barnaba alipopanda jukwaani na wimbo wake wa Milele, aliwakuta mashabiki hao wameshapagawa na yeye kuwaongezea mzuka kwa burudani ya nguvu. Mashabiki hao walizidi kupagawa zaidi baada ya Barnaba kumpandisha jukwaani Shishi Baby na kuimba nae pamoja wimbo mpya wa Shilole wa Hatutoi Kiki. Shishi Baby alimpisha Kala Jeremiah ambaye aliwakuta mashabiki hao wamewehuka kwa burudani, naye akaongeza ngoma juu ya ngoma.
Ukumbi ulirindima zaidi baada ya Nay wa Mitego kuvamia jukwaa kwa wimbo wake wa Muziki Gani, mashabiki wakavamia jukwaa huku baadhi wakitaka japo wamguse. Nay aliweka historia kubwa ndani ya ukumbi huo wa taifa wa burudani uliopo Mbagala jijini hapa alipowatendea haki mashabiki hao kwa kuwadondoshea ngoma zake zote mwanzo mwisho.
(PICHA/HABARI: ISSA MNALY/GPL)
0 Comments