NA HASSAN SILAYO-MAELEZO,KAGERA
Benki ya FINCA Microfinance imewasamehe mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 57.2 wateja wake 15 waliothibitishwa kuathirika kwa tetemeko la ardhi lililotokea terehe 10 mwezi huu mkoani Kagera.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Kanda wa FINCA Bw. Aluto Hagamu wakati akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu misaada kwa ajili ya waathirika wa Tetemeko la Ardhi Mkoani humo.
Hagamu alisema kuwa dhumuni kubwa la benki hiyo la kufuta mikopo hiyo ni kuwapunguzia mzigo wanachama hao kutokana na athari walizozipata kutokana na tetemeko hilo na kuwawezesha kurudi katika shughuli wanazozifanya ili kujiweka sawa kiuchumi.
Aidha, Bw. Hagamu kwa niaba ya benki hiyo pia wamekabidhi Sukari mifuko 25, mabati bando 5 pamoja na misumari katoni 8 kwa dhumuni kusaidia waathika wa tetemeko hilo.
Akitoa shukran baada ya kupokea misaada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu alizitaka benki nyingine kuiga mfano wa benki hiyo za kusaidia wanachama na waathirika wa tetemeko la ardhi kwa ujumla.
0 Comments