Serikali imevifungia vituo viwili vya redio nchini
kutokana na kurusha hewani taarifa za kichochezi zinazoweza kuchangia uvunjifu
wa amani.
Tamko la kufungwa kwa vituo hivyo
vya redio limetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
Nape alivitaja vituo hivyo kuwa ni
Kituo cha Redio Five cha Arusha na Kituo cha Redio Magic FM Dar es Salaam na alisisitiza kuwa
utekelezaji wa tamko hilo umeanza jana
Agosti 29, 2016 mara baada ya kutangazwa.
“Uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo
umefikia baada ya kujiridhisha kuwa kipindi cha MATUKIO kilichorushwa tarehe 25
Agosti ,2016 muda wa 02:00 usiku hadi 03:00 usiku na Kituo cha Utangazaji cha Redio Five
Arusha na kipindi cha cha Morning
Magic katika kipengele cha KUPAKA RANGI kilichorushwa tarehe 17 Agosti,
2016 kati ya saa 01:00 asubuhi na saa 02:00 asubuhi vilikuwa na maudhui ya
uchochezi unaoweza kuleta uvunjifu wa amani na hivyo kukiuka masharti ya kanuni
ya 5 (a),(b),(c) na (d) pamoja na Kanuni ya Huduma za Utangazaji (Maudhui) za
mwaka 2005”, alisema Nnauye.
Waziri huyo mwenye dhamana na vyombo
vya habari nchini alisema vituo hivyo vimefungiwa kwa muda usiojulikana na
ameelekeza Kamati ya Maudhui kuviita
vyombo hivyo na kuwasikiliza kwa kina
zaidi na kumshauri hatua zaidi za kuchukua kwa mujibu wa Kanuni za Utangazaji
za mwaka 2005.
Pamoja na hayo Nape
alivitahadharisha vyombo mbalimbali vya habari ,kutoshawishika kuvunja Sheria na
Kanuni zinazoongoza tasnia ya Habari ili
kulinda heshima ya tasnia ya habari na
kuhakikisha nchi inabaki na amani.
Hata hivyo Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya
mwaka 2003 Kifungu cha 28 (1) kimempa
Mamlaka Waziri wa mwenye dhamana na masuala ya Habari kufungia vyombo vya
habari vinavyoweza kurusha hewani habari za uchochezi.
0 Comments