Lilian Tungaraza 'Internet' akiwa katika pozi .
Imezoeleka kuona mtu akiagwa pale anapostaafu kazi
serikalini, kwenye sekta binafsi na kwingineko, na pia hivi sasa ni sawa na
jambo la kawaida kuona msanii akipotea kutoka kwenye steji na anapotafutwa
inaelezwa kwamba alishaacha usanii.
Lakini kwa mara ya kwanza katika tasnia ya unenguaji nchini,
uongozi wa kampuni ya African Stars
Entertainment (ASET) inayomiliki bendi ya Twanga Pepeta, umeandaa usiku maalum wa kumuaga mnenguaji wake mahiri,
Lilian Tungaraza, yule ambaye ni maarufu zaidi kwa mashabiki wa ‘minenguo’
nchini kama Lilian Internet.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Bongoweekend jijini
Dar es Salaam, Internet anasema ameamua kuacha unenguaji kwa ridhaa yake
mwenyewe na kutoka moyoni, hivyo hakuna yeyote aliyemshurutisha kwa namna moja
ama nyingine.
“Nimeamua kuacha kutokana na umri wangu kuwa mkubwa, hivyo
nawaachia hawa (vijana kama) kina Stella na wengineo waendelee na kazi
hii. Kwa hiyo natarajia kuwa onyesho
langu lililopangwa kufanyika Agosti 27 mwaka huu (ambayo ni Jumamosi wiki
ijayo) kwenye Ukumbi wa Mango Garden litakuwa la kukumbukwa”, anasema.
“Mimi ndiye nilimfuata Mama Asha Baraka na kumweleza kuwa
sasa ninahitaji kupumzika ili niwapishe wengine kwa sababu huu ni wakati wa
mabadiliko, siyo kwmba nimeshindwa kazi (hii) ya kunengua ila nimeamua
nistaafu”, ana ainisha.
Anaongeza kwamba bado yuko ‘fiti’ kwa namna zote kwenye
steji kiasi kuwa hata leo akiamua kupanda wenzie wanafahamu jinsi
atakavyowaonyesha kazi, lakini hatimaye uamuzi wake wa kupisha kando ndiyo huo.
Internet ambaye ubora wake wa kunengua umempa jina kubwa
‘Tizedi’ anabainisha kuwa amekuwepo stejini kwa miaka 19 hivi sasa, hivyo ana
mambo mengi ya kuweza
kumfanya awe kocha wa madansa ikiwemo kuwapa ushauri wake.
Nini kilichomvutia kunengua ?
Anasema alianza muziki kwa kuvutiwa na ‘masisteri’ wawili
‘mapacha’ waliokuwa wanenguaji ‘staa’ wa miondoko ya Nzawisa kutoka nchi
iliyokuwa Zaire wakati huo, ile ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Scola Miel na Betty Sumbu.
Mabinti hao kwa pamoja walikuwa katika kundi la L’Anti Choc
likiongozwa na Abuobakari Mbenzu Ngombani, yule ambaye wengi humuita kuwa Bozi
Boziana.
Bila shaka anazungumzia kipindi kile cha L’Anti Choc ya Response ya Lipapa ya Wara. Anazungumzia
kipindi kile ambacho kundi hilo ‘lilitesa’ na vibao vitamu na maridadi kama
‘Tembe na Tembe, Doukoure, Evelyn, Penitencier, Chama Chiko, Bissalu, Ebale,
Lucky’ na ‘C’est Pas Comme Ca’ vinavyobeba albamu ile ‘kali’ ya ‘Tembe na
Tembe’.
“Nilikuwa najifungia ndani ninaangalia mikanda yao ya video
na baada ya hapo nikitoka nacheza staili zao zote bila ya kukosea, jambo
lililosababisha niwe nakwenda kucheza kwenye shughuli mbalimbali kama harusi,
kipaimara na nyinginezo”, anasema alivyoanza mpaka kuwa mahiri kabisa wa
kunengua stejini.
Akiwa katika harakati zake hizo ndipo jirani yake mmoja
aliyeitwa Mama Sanda aliyekuwa mkubwa kuliko yeye alipomshawishi siku moja
kwenda naye kwenye ukumbi wa Silent Inn, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Anasema ilipofika ‘ofa’ ya watoto ‘kuidandia’ steji ili
kuonyesha vitu vyao ndipo nyota yake ikang’ara. Alicheza kwa namna zote mahiri
na kumvutia mwanamuziki aliyekuwa kiongozi wa bendi ya Ikibinda Nkoi wakati
huo, Ellystone Angai.
“Angai aliniita kando akaniambia amenikubali, hivyo
akaniambia niwe nakwenda kila Jumapili ambako bendi hiyo huwa inapiga dansi la
watoto na mimi nikaona hapahapa ndiyo njia, hivyo nikaitumia bila kufanya
ajizi”, anakumbuka vyema.
Anasema kipindi hicho cha mwaka 1998 alikuwa bado na miaka
17 tu, lakini aliamua kujikita zaidi
katika bendi hiyo iliyokuwa na wanenguaji wengine mahiri kama Salma Abeid,
Mamii Korando na wengineo.
Pamoja na kipaji alichokuwa nacho, Lilian anasema bado
alikuwa akienda kwenye maonyesho ya bendi hiyo kwa kujificha bila kuruhusiwa na
mama yake, lakini hatimaye akagundulika baada
ya kituo cha televisheni cha ITV kurusha
maonyesho ya bendi hiyo.
“Hapo mama yangu akaniambia kumbe wewe ndiyo maana umekataa
kusoma kwa sababu ya muziki? Haya endelea na hicho unachotaka na mimi nikaacha
rasmi shule na kujikita katika unenguaji wa bendi”, anasimulia.
Ilipofika mwaka 2001, Lilian alijiunga na bendi ya African
Stars na miondoko yake ya Twanga Pepeta ambako safu yao ya unenguaji ilikuwa
ikiundwa na yeye mwenyewe, Aisha Madinda na Halima White wote hao hivi sasa ni
marehemu.
Amefaidika na nini kutokana na kazi hiyo?
“Tukizungumzia tasnia ya sanaa kuna faida nyingi nilizopata.
Kwanza kabisa nimeweza kuisaidia familia yangu akiwemo mama yangu na wadogo
zangu, nimepata mume na watoto wawili. Nimeweza kuendesha maisha yangu
mwenyewe”, anajibu kwa utulivu na umakini mkubwa na kuendelea:
“Pia kwa kupitia muziki nimekuwa ni miongoni mwa wasanii
waliobahatika kwenda nchi mbalimbali kulikokuwa kunafanyika matamasha ya muziki
kama Oman, Dubai, Kenya, Uganda, Uingereza, Uholanzi, Sweden na Norway ambako
nimekwenda kwa sababu tu ya unenguaji”.
Anasemaje kuhusu Twanga
Pepeta?
“Nawashkuru ‘staff’ wote kwani nimeishi nao vizuri bila kumsahau mama ambaye ni Mkurugenzi wake
(akimaanisha Asha Baraka). Amenilea,
ameniozesha. Nashukuru kwamba nimekaa naye vizuri kwa muda wote huo”, anasema.
Nasaha kwa wanennguaji wenzake
Maisha ni kupigana, bila hivyo hakuna lolote linaloweza
kusogea. Lazima kuwepo pia na ubunifu, wasitegemee uongozi kwamba ndio utoe
maelekezo kwa ajili ya manufaa ya bendi. Mawazo mapya yanatakiwa kwa sababu
yatasaidia kupata mishahara pamoja na posho za kujikimu”, anawaasa wanamuziki
wanaobaki katika bendi hiyo iliyodumu kwa miaka mingi kati ya zote zinazotamba
na miondoko inayoitwa kuwa ya ‘bolingo’.
Kana kwamba haitoshi, Lilian anataka wasanii wote wajitume
zaidi kwa vile kupata jina siyo kitu cha mchezo. “Binafsi nimepewa jina hili la
Internet, sikulipata hivihivi ila nilijituma. Kuna vitu vingi ambavyo msanii
hupitia na yapo mazuri na mabaya, hivyo kwa kuwa na mimi ni kioo chao wachukue
mazuri yangu na kuacha mabaya”, anasema.
Changamoto alizoziona
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wanenguaji anasema
zipo nyingi ikiwemo jamii kuwadharau kwa kuona kwamba hawafai, lakini yeye
binafsi hajali akisema kuwa amefanya mambo mengi kutokana kwa sababu ya
kunengua stejini.
“Kwenye muziki sisi wacheza shoo tunadharaulika sana na mimi
mwenyewe nimewahi kutukanwa na mtu ‘live’ na wanaume ndiyo wanaongoza. Utaona
wakati wa kukutunza hakupi pesa mkononi, atakuwekea katikati ya makalio”,
anasema kwa huzuni.
Akifafanua kuhusu wanavyovaa wanenguaji, Lilian anasema kuwa
mavazi yao ni ya stejini na ya kikazi peke yake, lakini hawawezi kuvalia hivyo
wanapokuwa sehemu nyingine za kawaida huku akiongeza kwamba pindi wanaposhuka
tu kutoka kwenye jukwaa, kila mtu aanendelea na maisha yake ya kawaida yakiwemo
majukumu ya kifamilia.
“Hivyo ninachoweza kusema ni kwamba sitakuwa mbali na
masuala ya muziki. Ninaweza hata nikaanzisha kikundi changu cha madansa ambao
nitawafundisha kucheza na baadaye watakuwa wakitumika kwa mambo tofauti”,
anasema.
Naye Mkurugenzi na mmiliki wa bendi hiyo, Asha Baraka anasema kuwa tayari mashabiki wa Twanga
Pepeta wamepewa taarifa za onyesho hilo maalum, hivyo akaomba wadau mbalimbali
wajitokeze kwa wingi, Jumamosi wiki ijayo ili waweze kumuaga Lilian huku
akisema kwamba kutakuwa na mambo kadhaa ya kushtukiza.
“Internet ametumikia jukwaani kwa miaka 19, hivyo kwa kuwa
umri umesogea na yeye ni mama mwenye mume na watoto (wake) wawili ameamua
astaafu ili aweze kuitunza familia yake na maisha yake atayoyaendesha kwa
ujasiriamali”, anasema Asha.
Lilian mwenyewe anaongeza kuwa siku hiyo atapanda stejini na
kuonesha jinsi alivyo mahiri na mnenguaji mwenye kipaji kilichokuwa ndoto yake
ya tangu alipokuwa binti na mtoto.
Amelaani pia tabia ya baadhi ya vijana kuwa na idadi kubwa
ya wapenzi, lakini yeye anamshukuru Mungu kwamba ameweza kulipuka janga hilo
ambapo sasa ni mke wa mtu.
“Asilimia kubwa ya wanenguaji wanatumia dawa za kulevya siyo
kwa sababu ili wacheze vizuri jukwaaani, waliingia huko kwa kufuata mkumbo na
mimi jambo hilo silifurahii. Linaniumiza sana”, anasema gwiji huyo anayenengua
stejini kwa namna zote maridadi, kisha anaomba Mungu awasaidie ili kuondokana
na janga hilo.
0 Comments