Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) jana wametangaza
kumfungulia msanii wa muziki wa kizazi
kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego pichani juu kuendelea na
shughuli za Sanaa baada ya kuwa ametekeleza adhabu pamoja na maagizoyote aliyoelekezwa kama
masharti ya kumfungulia.
Akizungumza jana kwenye mkutano na waandishi wa habari
Katibu Mtendaji Godfrey Mngereza
alisema BASATA kama mlezi wa wasanii
linamfungulia kufuatia yeye mwenyewe Nay
wa Mitego kujutia na kukiri kwamba
amejifunza na yuko tayari kubadilika na kwamba hatarudia makosa aliyoyafanya.
Hata hivyo, pamoja na kumfungulia kuendelea na shughuli za sanaa
baraza linamweka kwenye uangalizi maalum msanii huyo kama sehemu ya kuhakikisha
anaendesha shughuli za sanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu sambamba
na kuzingatia maadili katika kazi zake.
“Itakumbukwa kwamba Julai 27 mwaka huu mwaka huu Baraza lilimfungia Nay wa Mitego kwa kipindi
kisichojulikana na kumtaka kutekeleza maagizo yafuatayo: kuhakikisha
amesajiliwa na kuwa na kibali cha
kuendesha shughuli za Sanaa,kulipa faini ya Shil.Mil. 1 , kuomba radhi
watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari na kwenye akaunti zake za
mitandao ya kijamii, kuufanyia marekebisho wimbo wa ‘Pale Kati’ ili ubebe maudhui yenye maadili” alisema
Mngereza.
Aidha msanii huyo ametekeleza
adhabu zote tajwa hapo juu , pia alikabidhiwa cheti chake cha usajili na kibali
cha BASATA.
Hata hivyo, pamoja na kuleta marekebisho mara mbili ya wimbo
wa ‘Pale Kati’ Baraza bado halijaridhishwa na marekebisho hayo hivyo
linaendelea kuufungia wimbo huu hadi hapo litakapojiridhisha umekidhi vigezo
vya kimaadili.
Katika kikao na msanii Nay wa Mitego cha kufanya tathimini
ya utekelezaji wa adhabu yake kilichofanyika Agosti 12 mwaka huu katika ofisi za BASATA ameagizwa kuendelea
kuufanyia marekebisho wimbo wake huo kama bado anaona anauhitaji.
Baraza linatoa maelekezo kwa vyombo vya habari na watanzania
kwa ujumla kuacha kuucheza wimbo huo hadi hapo itakapoelekezwa vinginevyo.
Hatua na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa chombo chochote cha habari
kitakachokiuka agizo hili.
Aidha, katika kikao hicho cha tathimini ilibainika kwamba Nay wa Mitego kwa taarifa potofu alizopewa
alipanda Jukwaani kwenye tamasha la Mwendo Kasi lililofanyika Julai 30 mwaka huu akiwa katika adhabu. Kwa kosa hili
ameandika barua ya kuomba radhi na Baraza linafikiria hatua za kuchukua kwa
waandaaji wa tamasha hili.
Baraza linatoa wito kwa wasanii kuendelea kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za sanaa sambamba na kuhakikisha
wanazingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili kuepuka matatizo yasiyo ya
lazima ambayo yanaathiri kazi zao kwa kiasi kikubwa sana.
0 Comments