Ofisa Habari wa BASATA , Aristides Kwizera
Wasanii
Kala Jeremiah na Super Nyamwela wanatarajiwa kupamba msimu mpya wa programu ya
Jukwaa la Sanaa ambayo imekuwa ikiendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni
(CAJAtz) kwa miaka mitano sasa tangu mwaka 2011.
Msimu
mpya wa Jukwaa la Sanaa unatazamiwa kuzinduliwa rasmi Jumatatu ya tarehe
25/07/2015 kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es
Salaam kuanzia saa saa 4:00 Asubuhi – 6:30 Mchana.
Wasanii
hawa wanatarajiwa kuupamba uzinduzi huo kwa kutoa burudani mbalimbali sambamba
na kuongea na wasanii wachanga katika kuwahamasisha na kuwajengea uwezo juu ya
namna wanaweza kutumia fursa mbalimbali za mashindano ya kukuza vipaji katika
kujijenga kisanaa.
BASATA
linatambua kwamba kumekuwa na tatizo la wasanii katika kutambua na kuchangamkia
fursa mbalimbali zilizoko katika sekta ya Sanaa hasa zile zilizomo kwenye
mashindano mbalimbali ya kutafuta vipaji ambayo wasanii Kala Jeremiah na Super
Nyamwela wamekuwa wakishiriki kikamilifu.
Ushiriki
wa wasanii hawa katika kuwajengea hamasa na kuwapa changamoto wasanii wachanga utasadia
katika kuwajengea uwezo wa kutumia fursa hizo.
Mbali
na burudani na elimu hiyo, uzinduzi huu wa msimu wa mpya wa Jukwaa la Sanaa
unaotarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya mia moja (100) utahusisha pia
kongamano maalum ambalo litajikita katika kutoa elimu mbalimbali kuhusu sekta
ya Sanaa kwa wadau watakaohudhuria.
Jukwaa
la Sanaa ni programu iliyobuniwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa lengo
la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya Sanaa lakini pia
kusaidia waandishi wa habari kupata habari zihusuzo sekta ya Sanaa kutoka
vyanzo mahsusi.
Imetolewa
na Kitengo cha Habari
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA)
0 Comments