Na Veronica Kazimoto
30 Mei, 2016.
Wito umetolewa kwa wadau pamoja na wananchi ili kushiriki
kikamilifu katika kuwezesha upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.
Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria
na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Dkt. Albina Chuwa amesema wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wana
mchango mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.
“Leo hii tumekutana na wadau mbalimbali wa Utafiti wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/2017 utakaofanyika mwezi
Agosti mwaka huu kwa ajili ya kujadili na kushauriana namna ya kufanya utafiti
huu kwa ufanisi ili kupata takwimu bora zitakazosaidia katika kutunga sera na
kupanga mipango ya maendeleo nchini”, amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amefafanua kuwa utafiti huu unategemea sana
ushiriki wa wananchi kwani wao ndio wadau na wahusika wakuu ambao wanapaswa
kutoa ushirikiano wa kutosha ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu rasmi
zitakazosaidia Taifa katika kuboresha huduma za afya kwa manufaa ya watanzania
wote.
Dkt. Chuwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ipo katika
harakati za kukamilisha maandalizi ya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI
Tanzania 2016/2017 ambao utaanza kufanyika nchi nzima kuanzia mwezi Juni mwaka
huu.
Aidha Dkt. Chuwa
amesema utafiti huu ni wa kipekee ukilinganishwa na tafiti
zilizotangulia kutokana na kuongezeka kwa viashiria vitakavyo chunguzwa ikiwemo
kuangalia kiwango cha CD4, kiwango cha maambukizi mpya, upatiakanaji wa huduma
zinazohusiana na UKIMWI pamoja na kupima watoto wadogo wenye umri chini ya
mwaka mmoja.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa utafiti huu kutasaidia
Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini hasa katika kupambana na
maambukizi mapya ya UKIMWI na namna ya kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa ICAP nchini, Dkt.
Fernando Morales amesema utafiti huu ni wa muhimu katika kupima viashiria na
matokeo ya UKIMWI kwa nchi ambazo zimekuwa zikipata msaada wa kupambana na
UKIMWI kutoka Serikali ya Marekani.
“Lengo la Utafiti huu ni kupata viashiria ambavyo
vinasababisha maambukizi mapya pamoja na kupima jinsi gani Taifa limeweza
kupambana na ugonjwa wa UKIMWI nchini”, amesema Dkt. Morales.
Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka
2016/2017 unafanyika katika nchi Ishirini (20) Afrika ambapo kwa sasa nchi nane
(8) zinaendelea na utafiti huu zikiwemo Zimbabwe, Zambia, Malawi, , Lesotho,
Swaziland, Uganda, Namibia na Tanzania.
0 Comments