Dk. Sophia Mlote, mkazi wa Kinyerezi Zimbili jijini
Dar es Salaam akiweka sawa vifaa mbalimbali kwenye banda lake la kilimo ambamo
amepanda nyanya. Dk. Mlote anatekeleza kilimo hai kupitia mradi wa Green Voices
unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa ambayo inaongozwa na
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, MarÃa
Teresa Fernández de la Vega
Bw. Abdon Hamaro, Ofisa Kilimo kutoka TAHA na mwezeshaji wa mafunzo ya akinamama
wa kikundi cha ‘Green Voices Kinyerezi’,
akiendelea kuwaelekeza wanakikundi (hawapo pichani) namna ya kuendesha kilimo
hai cha nyanya. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni Kinyerezi, jijini Dar es
Salaam.
Mratibu wa mradi wa Green Voices, Bi. Secelela Balisidya (kulia), akiwa
makini kuangalia Bw. Hamaro akiandaa mambo mbalimbali kwa ajili ya kuwaelekeza
wanakikundi namna bora ya kuendesha kilimo hai cha nyanya.
Wanakikundi cha Green Vocies Kinyerezi
wakifuatilia mafunzo hayo.
Christina Lwiza (kushoto) akipokea pakiti ya
mbegu ya nyanya kutoka kwa Dk. Sophia Mlote tayari kwa kuwatika ili kuanzisha
kilimo hai cha nyanya.
Bw. Hamaro akiandaa tray maalum kwa ajili ya
kuwapa wanakikundi kupandikiza mbegu kabla ya kupeleka kwenye vitalu vyao. Hii
ilikuwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo.
Wanakikundi wakijaza udongo maalum kwenye tray
kabla ya kuanza kupandikiza mbegu.
Bw. Hamaro akiwaelekeza kwa vitendo wanakikundi
namna ya kupandikiza mbegu hizo.
Hapa wanakikundi wakiendelea kupandikiza mbegu
kwenye tray.
10.
Banda maalum ambalo ni shamba muhimu kwa ajili ya kilimo hai (green house)
ambamo ndani yake nyanya zimestawi.
Picha ya pamoja ya wanakikundi cha Green Voices Kinyerezi.
NDANI ya banda kubwa lililoezekwa na kuzungushiwa plastiki
maalum katika Mtaa wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es Salaam, Dk. Sophia Mlote akiwa
ameongozana na mtaalamu wa kilimo, Bw. Abdon Hamaro, anaonekana akipanga vizuri
vifaa vya kilimo pembeni ya matuta yaliyostawisha vizuri nyanya.
Pembeni ya banda hili lenye ukubwa unaokadiriwa kuwa wa
meta 8 kwa 12, akinamama kadhaa wamezunguka wakitazama ustawi wa zao hilo huku
Bw. Hamaro akiendelea kutoa maelekezo ya namna ya kuendesha kilimo hai kinacholimwa katika mabanda maalum
yajulikanayo kama green houses ikiwa
ni sehemu ya mafunzo ya vitendo ya akinamama hao katika kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza kipato.
Tofauti na nyanya ambazo watu wamezoea kuziona zikilimwa
katika mashamba makubwa na bustani za wazi, nyanya hizi zinalimwa ndani ya
banda ambao ukubwa wake utategemea pia na eneo lililopo pamoja na uwezo wa
mhusika katika kulijenga banda hilo.
Hiki ni
kilimo hifadhi ambacho kinahimizwa kwa sasa ulimwenguni kote ili kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
“Mtu yeyote anaweza kuendesha kilimo cha mazao mbalimbali
kwa kutumia Green house hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam kama tunavyoona,
ni rahisi na rafiki wa mazingira kwa sababu unaweza kuendesha hata kwenye uwa
wa nyumba yako kama hivi,” Bw. Hamaro anaendelea kuwaeleza akinamama hao, ambao
ni wanakikundi wa mradi wa ‘Green
Voices’ unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa yenye makao
yake katika mji wa Madrid, nchini Hispania.
Mbali ya kutunza mazingira, Bw. Hamaro kutoka Chama cha
Wakulima wa Bustani Tanzania (TAHA) anasema, kilimo hai kinasaidia kuzalisha
vyakula visivyo na kemikali ambavyo ni rafiki wa afya ya binadamu.
Katikati ya Jiji la Dar es Salaam watu wamekuwa
wakishuhudia kilimo cha mboga mboga kwenye mabonde ya mito midogo, ambacho
kinatumia umwagiliaji wa maji machafu na yenye kemikali za kutoka viwandani,
ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.
“Mbegu zinazotumika zimetengenezwa maalum na hazifanani
za zile GMO zinazopigiwa kelele, lakini pia unatakiwa kutumia mbolea za asili
kama mboji na samadi, kwa sababu ukitumia kemikali nyingi kwenye udongo, mimea
inanyonya na kemikali hizo zinabaki kwenye vyakula na hatimaye kuingia miilini
mwetu,” anafafanua Hamaro.
Vile vile, Hamaro anasema kilimo cha Green house kinaweza
kutumika hata kwa matunda na kwamba kinatumia maji kidogo huku pia
kikimpunguzia gharama mkulima hasa kwa kuepukana na magonjwa mbalimbali ambayo
yanasababishwa na wadudu.
“Kwa kuwa banda limefunikwa na kukingwa, hakuna wadudu
waenezao magonjwa ya mimea wanaoweza kuingia, lakini faida nyingine ni kwamba,
unaweza kudhibiti hali ya hewa kwa kupunguza ama kuongeza joto ili kuifanya
mimea kukua vizuri,” anaongeza.
Dk. Mlote mwenyewe, ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika
Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo, ni mshiriki wa mradi wa Green Voices
ambaye baada ya mafunzo aliyoyapata, sasa anaieneza elimu hiyo kwa wanawake
wenzake majirani wa mtaa huo.
Yeyé ni miongoni mwa wanawake 15 waliopatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kupambana na
mabadiliko ya tabianchi ambayo yaliendeshwa nchini Hispania chini ya ufadhili
mkubwa wa taasisi ya Foundation for Women of Africa inayojihusisha na maendeleo
ya wanawake wa Afrika, ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania,
MarÃa Teresa Fernández de la Vega.
“Niliamua kuchagua mradi huu
kwa sababu, kwanza ni rahisi kuuendesha kwa kuwa shughuli zote zipo hapa
nyumbani na hata kama nitarudi usiku kutoka kazini, bado ninaweza kuingia humu
shambani na kuhudumia mimea kwa kuwa banda hili lina taa,” anaeleza.
Aidha, anasema, kwa kuwa
anakaribia kustaafu, na kwa elimu ya kilimo na uchumi aliyonayo pamoja na
utaalamu alioupata, ameona ni vyema aanzishe mradi ambao siyo tu utampatia
kipato, lakini pia utasaidia kutunza mazingira pamoja na kuwa msaada kwa jamii
kutokana na mazao yatakayovunwa.
“Niliamua kuwaelimisha wanawake
wenzangu katika mtaa huu na kuwashawishi waunde kikundi hiki na tayari
wamekwishapata mafunzo ya kutosha ambapo kila mmoja amekuja na wazo la
kuanzisha bustani ndogo nyumbani kwake ya mtindo huu kwa mazao ambayo anaona
yanafaa,” anaongeza Dk. Mlote, ambaye ameeleza kwamba, anakusudia kupanua
kilimo hicho kwa kupanda hata miti ya matunda.
Kikundi hicho cha ‘Green Voices
Kinyerezi’ kinaundwa na wanawake 10, ambapo mbali ya kujifunza kwa nadharia
namna ya kuendesha kilimo hai kwa njia ya green house, walipata fursa ya
kufanya kwa vitendo kwa kupandikiza mbegu za mazao mbalimbali ya mboga mboga
kama nyanya, kabichi, hoho, matango na matikiti maji kwenye bando hilo ambapo
yatakapoota kila mmoja atakwenda kupanda nyumbani kwake.
Christina Lwiza, mmoja wa wanakikundi hicho ambaye anajishughulisha na
biashara ya uuzaji vinywaji kwenye grocery yake mwenyewe, anasema ameshawishika
kuanzisha kilimo cha nyanya nyumbani kwake ambacho kinaweza kumpatia mapato ya
nyongeza pamoja na kukidhi mahitaji ya nyumbani.
“Sijawahi kulima nyanya, lakini kwa mafunzo niliyoyapata, hakika naweza
kuendesha kilimo hicho bila shida,” anasema Christina.
Karibu wanakikundi wote wamehamasika, ambapo kila mmoja ameamua kubuni
zao ambalo linaweza kumfaa.
Mratibu wa mradi huo, Bi. Secelela Balisidya, anasema mradi huo wa kilimo
hai cha nyanya kwa kutumia green house ni sehemu ya miradi 10 inayoendeshwa
nchini Tanzania kupitia Green Voices ambapo inaendeshwa katika mikoa sita ya
Tanzania Bara.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam,
Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro ambapo inahusisha kilimo,
usindikaji, ufugaji na utafiti.
“Miradi hiyo ni kilimo cha miti
ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani
Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa
kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali
kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, kilimo cha uyoga
mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti
wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro,” amefafanua Secelela
Balisidya.
Aidha, amesema kwamba, lengo
kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao
wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya Kitanzania iweze
kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya
tabianchi.
Mradi huo unatarajiwa
kutelekezwa kwa mwaka mmoja ili kutoa fursa kwa akinamama kutoa ujuzi wao wa
kupambana na mabadiliko ya tabianchi na sauti zao kusikika, kwa sababu kazi wanazozifanya
kila siku za kilimo na utunzaji wa familia zinahusiana moja kwa moja na
mazingira hivyo kuyaelewa zaidi mazingira na jinsi ya kupambana na mabadiliko
ya tabianchi.
Malengo ya dunia
Kilimo hai kinaendana na masuala mtambuka ya mazingira
pamoja na kukabiliana na uhaba wa chakula na kupunguza umaskini kama
inavyoelezwa kwenye Malengo Endelevu ya Dunia yaliyopitishwa mwaka 2015.
Kwa mujibu wa malengo hayo, mataifa mbalimbali
yamekubaliana kuhakikisha yanatokomeza umaskini kwa namna zote pamoja na
kukomesha njaa na kupata uhakika wa usalama wa chakula na kuboresha lishe kwa
kuhimiza kilimo endelevu.
“Kilimo hai ni endelevu kwa sababu unaweza kulima wakati
wowote hivyo kinaweza kukabiliana na njaa na uhakika wa chakula ni mkubwa,
lakini pia kitasaidia familia kuongeza kipato kwa kuuza ziada ya chakula kitakachozalishwa,”
anasema Hamaro.
Lakini pia kwa kutumia kilimo hai, lengo namba sita la
dunia linaweza kutimia, kwani ni kilimo ambacho kinatumia maji kidogo, hivyo
kuhakikisha utunzaji mzuri wa vyanzo vya maji na matumizi sahihi ya maji
yaliyopo.
Aidha, kilimo hai pia kinaweza kukidhi lengo namba 13 la
dunia linalohimiza kupambana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake
Sera ya Kilimo
Kilimo hai ni sehemu ya mapendekezo yanayotajwa kwenye
Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 ambayo inaendana na Dira ya Taifa ya
Maendeleo kuelekea mwaka 2025 kwa kuhimiza kilimo chenye tija pamoja na
utumiaji mzuri wa rasilimali zilizopo, hususan ardhi na maji.
Kwa maana nyingine, kuhamasisha kilimo hai ni sehemu ya
utekelezaji wa malengo, dhima na dira ya sera hiyo hasa katika kipindi hiki
ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko
ya tabianchi, ambayo serikali pia imeainisha mikakati yake katika Sera ya Taifa
ya Mazingira ya mwaka 2007.
0 Comments