TAARIFA YA CCM JUU YA KUFUNGA KAMPENI ZAKE KATIKA MIKOA MBALI MBALI

CCM inapenda kutoa taarifa kuhusu masuala kadhaa kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wake na kwa umma wa Watanzania.
Kufunga Kampeni
CCM itafunga kampeni zake kwa utaratibu mpya na kwa kishindo. Kampeni za CCM zitafungwa Kitaifa kwa mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa mitano. Mikutano hiyo itaongozwa na viongozi wa CCM Kitaifa waliopo madarakani na wastaafu. Mikoa hiyo na viongozi watakaoongoza mikutano hiyo ni kama ifuatavyo:
1. Mwanza – Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, Mgombea Urais, na Ndugu Samia Hassan Suluhu, Mgombea Makamu wa Rais
2. Tanga – Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
3. Mbeya – Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
4. Mtwara – Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
5. Kigoma – Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
6. Kilimanjaro – Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu
7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu
Kati ya leo na kesho, maeneo mengine yanaweza kuongezeka. Mikutano hii itaanza saa sita mchana na itarushwa, yote kwa pamoja, kwa matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni vitano na vituo vya redio 67. Vilevile, watakaohudhuria katika mikutano hii wataunganishwa moja kwa moja na mkutano wa Mwanza, alipo Mwenyekiti, Mgombea na Mgombea Mwenza, na wataweza kusikiliza hotuba ya Dkt. Magufuli moja kwa moja kupitia screens zitakazokuwa katika viwanja vyote hivi saba.
Namna hii ya ufungaji wa kampeni itakuwa ni ya kihistoria, na inadhihirisha nguvu ya CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa ya kampeni kwa siku moja katika maeneo mbalimbali nchini. Lakini pia tutaweka historia katika tasnia ya utangazaji wa televisheni hapa nchini kwa kutangaza na kuunganisha kwa pamoja matukio saba kwa wakati mmoja.
Kwa upande wa Dar es Salaam, tutafanya mkutano mkubwa wa ufungaji wa kampeni za Mkoa wa Dar es Salaam, katika Uwanja wa Jangwani, kesho, Ijumaa, tarehe 23 Oktoba 2015. Siku ya Jumamosi, tarehe 24 Oktoba 2015, Wagombea Ubunge katika majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam watafunga kampeni katika maeneo ya majimbo yao kwa namna mahsusi.
Tathmini ya Kampeni
Kama Chama, tumeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni tulizofanya licha ya changamoto za hapa na pale. Dkt. Magufuli na Ndugu Suluhu wamefanya kazi kubwa, na kwa bidii kubwa, na maarifa makubwa. Wamekuwa barabarani kwa siku 57 wakifanya mikutano kati ya 8 hadi 12 kwa siku. Imani yetu ya ushindi inatokana na kazi kubwa waliyofanya. Pia, CCM inawashukuru viongozi, wapenzi wa washabiki wake – wa makundi mbalimbali ya kijamii - kote nchini kwa kazi kubwa ya kampeni waliyoifanya.
Kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanyika, na kutokana na mwenendo wa tafiti huru na tafiti zetu za ndani, CCM inategemea ushindi wa asilimia zisizopungua 69.
Uchaguzi wa Amani
CCM haitachoka kuendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na utulivu. Sisi kama chama kikubwa cha siasa nchini, chenye wafuasi wengi zaidi, na chenye dhamana ya uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu wa kuhimiza utulivu kwa wapenzi, washabiki na wanachama wetu. Tunawataka na wenzetu wafanye hivyo.
Kauli za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za kutojiamini na kujiandaa kufanya vurugu. Kauli za kwamba washabiki wa UKAWA wakishapiga kura wabaki vituoni kulinda kura si kauli za wanaotaka uchaguzi wa amani.
Kwa utaratibu wetu wa uchaguzi, utaratibu wa pekee kwa Chama kulinda kura zake ni kwa kupitia wakala wa vyama waliopo kwenye kila kituo cha kupiga kura na wenye nguvu na mamlaka ya kisheria ya kushuhudia zoezi zima, kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura hadi kutangaza matokeo. Kura zinapigwa na kuhesabiwa vituoni mbele ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Mawakala wa vyama na Waangalizi wa Uchaguzi wa ndani na nje ya nchi. Mawakala wa vyama na Wasimamizi wa Uchaguzi wanaweka sahihi kwenye fomu za matokeo, na matokeo hayo yanatangazwa na kubandikwa kwenye kituo. Kwenye kituo kikuu cha Tume cha kujumlisha matokeo, mawakala wa vyama pia huwepo na Tume hujumlisha matokeo kutoka kwenye fomu za matokeo za vituo vya nchi nzima zilizosainiwa na mawakala wa vyama kwenye kila kituo. Kwa viongozi wa UKAWA kuwaambia watu waingie barabarani au kuvizunguka vituo vya kupigia kura eti ili kulinda kura hakuna maana yoyote zaidi ya kutafuta namna ya kuhalalisha fujo, vurugu na uporaji na kuwazuia watu wengine, hasa wanawake, kupiga kura. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vizuie hili jambo kwa sababu halina nia njema.
Mkakati wa UKAWA ni kufanya vurugu baada ya kushindwa na kutengeneza mazingira ya mgogoro wa kisiasa ili Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati na kupendekeza kugawana madaraka. Mkakati huo hautafanikiwa. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe ulinzi na usalama wa watu wote na mali zao siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
CCM haitakubali hata kidogo ushindi wake kuhojiwa au kutiliwa shaka kwa sababu tu ya vurugu zilizoanzishwa na watu wengine.
Siku ya Jumamosi, CCM itatangaza namba maalum za simu kwa Watanzania wote ili siku kabla ya Uchaguzi, siku ya Uchaguzi na mara baada ya uchaguzi, waweze kupiga simu au kutuma ujumbe pale watakapokuwa wanabaini au kushuhudia vitendo vya kuvuruga amani na kuvuruga utaratibu mzima wa Uchaguzi.
Kupokea Matokeo
CCM imeweka utaratibu wa kupokea matokeo kwa kutumia Mawakala wake moja kwa moja vituoni na kupitia mtandao wa Chama. CCM inategemea kuwa na matokeo ya Uchaguzi nchi nzima ifikapo saa nne usiku, siku ya Uchaguzi, tarehe 25 Oktoba 2015.
Imetolewa na:
January Makamba
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
MJUMBE WA KAMATI YA KAMPENI
22 OKTOBA 2015.

Post a Comment

0 Comments