Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dkt. Albina Chuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa
sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge Mwezi Machi mwaka
huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi
hiyo Bw. Morrice Oyuke
na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu
ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 .
Na Veronica Kazimoto.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Sheria Mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 haina
lengo la kuzuia Taasisi au watu binafsi kufanya tafiti zao hapa nchini bali
inalenga kuweka misingi imara ya shughuli za kitakwimu na tafiti zenye
ulinganifu unaotokana na mfumo rasmi utakaoondoa uwepo wa takwimu
zinazokinzana.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari
kuhusu ujio wa sheria hiyo mpya iliyoridhiwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu.
Amesema
kuanzishwa kwa sheria hiyo kunalenga kutoa mwongozo kwa Taasisi za Serikali na
Mashirika mbalimbali yanayozalisha takwimu hapa nchini ili yaweze kuendesha
shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa takwimu kwa kuzingatia sheria hiyo mpya
na kuwa huru kutoa takwimu sahihi zinazoendana na uhalisia wa Tanzania.
“Sheria
hii hailengi kuondoa uhuru wa taasisi nyingine za utafiti za utafiti zilizopo
kisheria kufanya kazi zao, taasisi hizo zitaendelea kuwa huru kufuata taratibu
zao ilimradi hazikiuki sheria hii” Amesisitiza Dkt.Chuwa.
Amefafanua
kuwa kifungu cha 20 cha sheria hiyo,kinaeleza kuwa takwimu zinazotolewa na
taasisi zilizo nje ya Serikali lazima zikidhi vigezo vya kitakwimu vilivyowekwa
na NBS ili ziweze kutumika kupanga mipango ya maendeleo.
Kuhusu
wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofanya tafiti mbalimbali chini ya wahadhiri wa vyuo
vikuu Dkt. Chuwa amesema ipo sheria inayowalinda na kusimamia matokeo ya tafiti
zao zinazosambazwa kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha
vyuo vikuu.
Ameongeza
kuwa sheria hiyo katika kifungu cha 37 (3) imeainisha makosa mbalimbali na
adhabu ya kifungo kisichopungua miezi 6 au faini isiyopungua shilingi milioni
moja.
Ameyataja
makosa hayo kuwa ni upotoshaji wa ukweli kuhusu takwimu rasmi utakaofanywa na
vyombo vya habari, vitendo vya kuzuia msimamizi, mdadisi au karani wa Sensa
kutekeleza majukumu yake kisheria,kukataa kwa makusudi kujaza fomu au nyaraka
yoyote au kujibu maswali yaliyoulizwa, kutoa taarifa zisizo sahihi, kuharibu
fomu au nyaraka yoyote na mtu yeyote kujifanya msimamizi , mdadisi au karani wa
Sensa kwa lengo la kupata taarifa ambazo hastahili kuzipata.
Makosa
mengine ni yale ya kushawishi mtu asishiriki katika zoezi la kitaifa Kitakwimu
litakaloendeshwa na Ofisi hiyo kwa mujibu wa sheria hiyo, kukataa kutoa nyaraka
zozote zinazohitajika katika shughuli za kitakwimu na kukiuka kifungu chochote
cha sheria hiyo.
Kuhusu
mchakato wa kupatikana kwa sheria hiyo amesema umezingatia vigezo vyote ikiwemo
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha muswaada wa Sheria ya
Takwimu ya mwaka 2015 katika Mkutano wake wa 19 na kisha kujadiliwa Bungeni,
Muswaada huo kuwasilishwa kwa wadau ambao waliujadili na kutoa maoni ambayo
yalisaidia kuboresha muswaada huo.
Amesema
kuwa kutakuwa na kamati maalumu ya kitaalam itakayoundwa kwa ajili ya kuangalia
takwimu zitakazokuwa zinakusanywa ili kuhakikisha kuwa hakuna ukiritimba wowote
unaojitokeza katika kuthibitisha na kupitisha tafiti na takwimu
zitakazowasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Amesisitiza
kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo
kuzumgumza na vyombo vya habari ili kujenga uelewa wa umuhimu wa sheria hiyo
kwa maendeleo ya Taifa.
0 Comments