Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Hashim Lundenga ambao ndiyo waandaaji wa shindano la Miss Tanzania
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limeushangaa uongozi wa
Kampuni ya Lino International Agency ambao ni waandaaji wa shindano la Miss
Tanzania, kukurupuka na kwenda kukata rufaa kupinga kufungiwa kwa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni Michezo na Utamaduni, kwani wangeweza kubaki barazani
na kuzungumza nao.
Baraza hilo lilisimamisha shindano hilo kwa miaka miwili
kutokana na waandaaji kukiuka kanuni, ikiwamo mawakala kutokuwa na vibali
kutoka Basata, kabla ya wahusika kuamua kuandika barua kwa Waziri mwenye
dhamana na michezo, Dk. Fenella Mukangara, kupinga adhabu hiyo.
Akizungumza Ofisini kwake Ilala
Sharif Shamba jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey
Mngereza, alisema Kamati ya Miss Tanzania chini ya Kampuni ya Lino
International Agency, inatakiwa kujipanga upya katika kuandaa shindano lenye
ubora ili watakapotoka kifungoni waje na sura mpya kutokana na kushuka kiwango
siku baada ya siku.
Alisema Miss Tanzania walipaswa kukaa na waandaaji wao na
kuwaeleza kilichotokea, halafu wangechanganya mawazo kwa kushauriana, kwani
penye wengi pana mengi.
“Baada ya Basata kutoa tamko la kuwataka Lino wajipange na
kuweka sawa changamoto zilizojitokeza ambazo wao wanazijua kwa undani zaidi...Tulitegemea
Kamati ya Miss Tanzania ingekutana na wadau wake ikiwa ni pamoja na wakala wake
wa mikoa kadhaa kama siyo wote, ambao wangewawakilisha wengine ili waweze
kuchanganua na kutafakari adhabu waliyopewa, kwa sababu suala hili siyo la mtu
mmoja mmoja,” alisema Mngereza na kuongeza.
Tunatambua kwamba shindano hili la urembo nchini lina mashabiki
wengi, pia huzalisha ajira nyingi, kwa sababu hata hao warembo wenyewe ambao
ndiyo huwa washiriki nao wako pale kwa sababu ya kupata riziki ambayo hutolewa
na waandaaji kama zawadi na kifuta jasho...Pia ajira zingine hupatikana kwa wenye
kumbi, wasanii, wenye vyombo vya miziki, wauza vinywaji na hata wakaanga chipsi
nao huo huwa ni msimu wao, lakini wote tunapaswa kufuata taratibu.
Alibainisha kuwa, hitaji kubwa la Basata kutoka Miss
Tanzania ni kuona mfumo wa uandaaji na muendeshaji umebalilika, kamati inaundwa
kwa kuzingatia jinsia hasa wanawake, ambako hivi sasa hilo halipo.
“Waandaaji wangekuja na mkakati mpya wa kuandaa shindano
hilo, tungekaa mezani na kushauriana
nini kifanyike, wapi wamekwama ili shindano lirudi katika hadhi yake...Ni
ukweli lilishuka hivyo tunaamini kwamba hili jambo endapo likitiliwa mkazo basi
Miss Tanzania watarudi katika hadhi yao.
“Lino wajipange na kutatua changamoto na kuboresha mfumo
mzima wa uandaaji, hasa zile wanazozifahamu kwani hata jamii inazijua baadhi ya
changamoto hizo, ikizingatiwa hivi sasa tuko nje ya wakati wa uandaaji,
nasisitiza waje na mpango mpya ambao utaonyesha matumaini na imani yetu ni
kwamba wataleta, japo hadi hivi sasa hawajaleta mpango wowote mpya,” alisema
Mngereza.
Pia, ameitaka kamati iweke wazi mikataba yake na warembo,
wazazi wa warembo washiriki wanapaswa kushirikishwa na kuridhia, hivyo
wajipange zaidi kuliko kukaa na kumtafuta mchawi, shindano ni lao na halitapewa
mtu mwingine ama taasisi nyingine kuratibu.
“Sisi Basata tumefuata ‘process’ zote, hivyo hakuna suala la
kufungulia shindano kwa masharti mapya, kwani hata mimi nilisoma kwenye vyombo
tofauti vya habari kwamba Basata imefungulia shindano la Miss Tanzania,
hatuwezi kuwafungulia kimya kimya...Jinsi tulivyowasimamisha kwa barua na
kutangaza kwenye vyombo vya habari, ndivyo hivyo hivyo tutakavyo wafungulia,”
alisema.
Aidha, amewataka Miss Tanzania wasionge hatua iliyochukuliwa
na Basata kuwa ni uonevu kwao, bali wachukulie kama ni kipindi cha wao
kujipanga vizuri zaidi kwa program yao huku akiwataka wadhamini wawe na imani
na shindano hilo kwa ujumla.
Chanzo cha shindano hilo kufungiwa ni baada ya kuibuka kwa madai
kuwa mshindi taji hilo, Sitti Mtemvu, kadanganya umri wake pia kamati
ikashindwa kuthibitisha umri sahihi, jambo ambalo likafanya Basata wakaamua kulichimba
zaidi shindano hilo na mwisho wakatoka na uamuzi wa kulifungia shindano kwa
miaka miwili na kuwataka wajipange upya.
0 Comments