VIINGILIO MECHI YA SIMBA NA YANGA VYATAJWA


Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania,Boniface Wambura akizungumza na wanahabari,wakati akitangaza viingilio na utaratibu wa kuingia uwanjani katika Mechi ya Watani wa Jadi,Simba na Yanga unaotaraji kuchezwa Oktoba 18,2014 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Picha na Othman Michuzi.
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba itakayochezwa Jumamosi (Oktoba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 7,000.

Washabiki watakaolipa kiingilio hicho ni wale watakaokaa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo jumla yake ni 36,693 katika uwanja huo wenye viti 57,558. Viingilio vingine ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.

Tiketi zitakazotumika kwenye mechi hiyo ni za elektroniki, na zimeanza kuuzwa jana (Oktoba 13 mwaka huu). Tiketi zinapatikana kwa mtandao wa M-PESA, CRDB Simbanking na maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo zaidi ya mia moja sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo namba 27 itakayochezeshwa na mwamuzi Israel Mujuni Nkongo akisaidiwa na John Kanyenye na Ferdinand Chacha itaanza saa 10 kamili jioni. Kamishna wa mechi hiyo ni Salum Kikwamba kutoka mkoani Kilimanjaro.

Washabiki wanatakiwa kununua tiketi mapema, kwani hazitauzwa uwanjani siku ya mechi. Milango yote ukiwemo ule wa upande wa Mbagala (Uwanja wa Ndani) itafunguliwa kwa ajili ya washabiki, na itakuwa wazi kuanzia saa 4 asubuhi.

Magari maalumu tu yenye stika ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kupitia Barabara ya Mandela. Pia washabiki hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakiwa na silaha, vitu vya vyuma na mabegi makubwa. Barabara ya kuingilia upande wa Chang’ombe itafungwa kwa watumiaji wa magari.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Post a Comment

0 Comments