Mratibu wa Uhuru Marathon Innocent Melleck akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa mbio hizo mwaka huu ambapo zitafanyika 07/12/2014 kwenye viwanja vya leaders Club jijini Dar Es Salaam kulia kwake ni Naibu Katibu mkuu wa wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na michezo Profesa Elisante Ole Gabriel.
NA BONGOWEEKEND REPORTER
MASHINDANO ya mbio nefu za Uhuru Marathon
ambayo yamepangwa kufanyika Desemba 7 mwaka huu yamezinduliwa rasmi jana jijini
Dar es Salaam kwa kuwataka wanariadha kujitokeza ili kuimarisha Amani,afya,
uhuru, uzalendo na muungano wa Watanzania.
Akizungumza jana jijini, Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof Elisante Ole
Gabriel , alisema kuwa anaipongeza Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo kwa sababu
zinalengo la kihistoria la kumbukumbu za Uhuru wa Tanzania.
Elisante aliwaomba wahisani mbalimbali kujitokeza kwa wingi na kudhamini mbio
hizo huku akisisitiza kuwa serikali ipo bega kwa bega katika kuhakikisha ujumbe
wa mwaka huu unawafikia walengwa ambao ni jamii nzima ya kitanzania na wapenda
amani wote ulimwenguni.
Ndugu
zangu serikali inawaomba kwa dhati kabisa watu na mashirika mbalimbali ya
kiserikali na mashirika binafsi kujitokeza kwa wingi katika kudhamini mbio hizi
kwa kuwa lengo lake ni chanya kwa taifa letu,hata pale serikali itakapohitajika
kutoa ushirikiano wowote basi kama serikali tupo tayari kwa hilo muda wowote ,
Alisema kuwa kupitia mbio hizo suala la
Amani litasisitiza na hakuna mahali popote duniani ambapo wananchi wake
hawapendi Amani.
“Mbio hizi zinafanyika huku jambo muhimu
likiwa ni kusisitiza na kuuenzi Muungano wetu katika jamii iliyostahamilivu,”
alisema kiongozi huyo wa wizara.
Aliwataka pia wenyeji wa mbio hizo, Chama
cha Riadha mkoa wa Dar es Salaam (DAAA) kusimamia kikamilifu mbio hizo kwa
sababu ni sehemu ya kuwaandaa wanariadha na mashindano mengine ya kimataifa
watakayoshiriki.
Mratibu wa mbio hizo, Innocent Melleck,
alisema kuwa mbali na kuendeleza vipaji vya wanariadha, mbio za Uhuru Marathon
zina lengo la kuhamasisha Amani, umoja na mshikamano wa wananchi wa Tanzania.
Melleck alisema kuwa kupitia mbio hizo
pia wananchi watashiriki kusisitiza Muungano uliopo hapa nchini.
Alisema kuwa anaamini mbio za mwaka huu
zitasaidia kuutangaza mchezo wa riadha ambao miaka ya nyuma uliipa sifa kubwa
Tanzania kwa wanariadha wake kupata medali katika mashindano ya kimataifa.
Aliongeza kuwa katika mbio hizo,
wanariadha watachuana katika marathoni, nusu marathoni na mbio maalumu za
kujifirahisha za kilomita tano.
Melleck aliitaja kauli mbiu ya mbio za
mwaka huu ambazo zitaanzia kwenye viwanja vya Leaders jijini ni “ Uhuru Wetu, Amani
Yetu, Tuitunze”
Naye Katibu Msaidizi wa DAAA, Ombeni
Zavalla, alisema kuwa chama hicho kiko tayari kushirikiana na Kamati ya
Maandalizi ili kufanikisha mbio hizo zinafanyika kwa kufuata taratibu zote za
kiufundi.
Mbio
za uhurumarathon zinafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo hapa nchini ambapo
mwaka jana zilifanyika tarehe 08/12/2013 hapa jijini Dar Es Salaam ambapo mgeni
rasmi alikuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Mohamed
Gharib Bilal ambapo jumla ya wanariadha 2618 walishiriki mbio hizo toka katika
mataifa 21 .
0 Comments