WASANII WASISITIZWA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO YA KIJAMII

Mdau wa Sanaa Henry Mdimu (Kulia) akisisitiza umuhimu wa kuwa na mitandao ya kijamii kwa wasanii (hawapo pichani) katika Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Kushoto ni Afisa Sanaa wa BASATA, Augustino Makame.
 Afisa Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristides Kwizela (Kulia) akisisitiza jambo kwa Wasanii (Hawako pichani) wakati wa Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Katikati ni mdau wa Sanaa Henry Mdimu na Afisa Sanaa wa Baraza hilo Augustino Makame.
Na Mwandishi Maalum
Wasanii wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwani waandaaji wa matamasha na matukio mbalimbali ya kisanaa sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakiitumia katika kuwapa kazi.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam, mdau wa Sanaa Henry Mdimu alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakitumia kurasa zao kuonesha mambo binafsi kama ya mapenzi na matusi wakati zinapaswa kutumika kwa ajili ya kazi zao za Sanaa na kuwasiliana na mashabiki wao.
Alisisitiza kwamba si kila kitu kinapaswa kuwekwa kwenye kurasa za kijamii za wasanii na kwamba lazima wasanii wajifunze kutenganisha maslahi au masuala yao binafsi dhidi ya yale ya wapenzi wao na kwamba Sanaa iko kwa ajili ya walaji na si wasanii pekee.
“Wasanii hawana budi kuelewa kuwa hawatengenezi sanaa au kurasa za mitandao ya kijamii kwa ajili yao. Wanaitengeneza ili kuwasiliana na mashabiki wao kuhusu kazi wazifanyazo na kutafuta fursa za masoko na kazi nje. Lazima waelewe mapromota wa kimataifa hutumia sana kurasa hizi katika kutoa fursa” alisisitiza Mdimu.
Aliongeza kwamba, msanii yeyote anayefanya kazi ya Sanaa kama kazi yake lazima afikirie kutumia mitandao hii ya kijamii kiweledi katika kujitangaza kwani kutokufanya hivyo ni bora kufanya kazi nyingine maana hiyo ndiyo njia kuu kwa sasa ya kujitangaza na kupata fursa za maonesho mbalimbali ya kimataifa kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Afisa Sanaa kutoka BASATA, Augustino Makame alisema kwamba Baraza limekuwa mstari wa mbele kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia za kupashana habari muiongoni mwa wasanii na kwamba sasa ni muda wa wasanii kuona umuhimu wa mitandao hii ya kijamii na kuitumia ipasavyo katika kukuza Sanaa zao.

Post a Comment

0 Comments