Emmanuel Okwi (kushoto) akifanya vitu vyake jana dhidi ya Gor Mahia
Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imekutana leo (Septemba 7 mwaka huu) na kupitia masuala
mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na
mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba
huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na
upande wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo
umevunjika.
Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
Yanga
ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia
Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa
maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu
yoyote.
Mkataba
ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati
imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo
mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.
Pamoja
na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao
kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa
kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi,
na si usajili.
Pia
lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri.
Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na
kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Hata
hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi.
Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na
suala la kupiga kura.
Kuhusu
pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu
hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa
mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake.
Vilevile
Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika
mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa
kulipa ada hizo.
Pia
Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia
uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi,
vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi watakapolipa.
Mashauri mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya kamati.
0 Comments