Jamii
imetakiwa kujenga tabia ya kuchangia damu kwa hiari kitendo ambacho
kitapunguza vifo vya kina mama wajawazito 363 vinavyotokea kila mwaka
kutokana na tatizo la ukosefu wa damu wakati wa kujifungua.
Mwito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na
wananchi wa mkoa wa Kigoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya
wachangia damu Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani humo.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema takwimu zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya
vizazi hai laki moja hufa kila mwaka kutokana tatizo la uzazi na
asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa damu.
“Ni
dhahiri vifo vinavyotokana na uzazi viko juu na kwa bahati mbaya
waathirika wakubwa ni wasichana chini ya umri wa miaka 15, makundi
mengine yanayohitaji kuongezewa damu ni kina mama wajawazito wakati wa
mimba na kujifungua , watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa
ukosefu wa damu unaosababishwa na malaria kali na magonjwa mengine,
ajali, wagonjwa wa saratani, upasuaji mkubwa wa moyo, anemia, seli mundu
na hemophilia.
Ni
wajibu wetu sote kuhakikisha kwamba tunatoa damu ili jamii yetu iweze
kutimiza mahitaji yake kwani tunapokuwa na akiba ya damu iliyo salama
tunajihakikishia tiba ya ndugu zetu pale wanapopata matatizo bila ya
siye kulazimika kutoa damu ya papo kwa hapo”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti
hiyo wa WAMA alisema mtu yeyote mwanamke au mwanaume anaweza kuchangia
damu ikiwa ana afya njema, umri kati ya miaka 18 hadi 65, uzito
usiopungua kilo 50, uwingi wa damu zaidi ya gramu 12 kwa desilita,
kutokuwa na shinikizo la damu na kwa mwanamke asiwe mjamzito au
ananyonyesha.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Stephen Kebwe
alisema tangu kuanzishwa kwa mpango wa damu salama mwaka 2004 kumekuwa
na ongezeko la wachangia damu kwa hiari kutoka kiasi cha chupa 5000 kwa
mwaka 2005 hadi chupa 160000 kwa mwaka 2013.
“Changamoto
zinazoukabili mpango huu ni mahitaji makubwa kuliko upatikanaji wa damu
inakadiriwa mahitaji ya damu kwa mwaka kitaifa ni wastani wa chupa
400000 hadi 450000, uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala zima la
uchangiaji damu kwa hiari, uuzwaji wa damu usio halali Hospitalini jambo
ambalo linakatisha tamaa wachangia damu wa hiari na matumizi yasiyo
sahihi ya damu katika Hospitali”, alisema Dkt. Kebwe.
Naibu
waziri huyo wa Afya na Ustawi wa Jamii alisema mpango wa taifa wa damu
salama unaendelea kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji wa damu
katika jamii, kuendelea kujenga vituo vidogo vya kuchangia damu, kutoa
majibu, nasaha, na malezi kwa wiki mbili mpaka nne baada ya mtu
kuchangia damu na kuongeza mazao mbalimbali ya damu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali
Mstaafu Issah Machibya aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kujitoa
kwao katika zoezi zima la uchangiaji wa damu salama na kuweza kukusanya
chupa 3620 kwa kipindi cha wiki tatu kabla ya kilele cha maadhimisho hayo
na hivyo kuvuka malengo kwa asilimia 121 kwani kabla ya kuanza kwa
zoezi hilo walijipangia kukusanya chupa salama za damu 3000.
“Mkoa wa Kigoma hupata Damu salama kutoka
kituo cha Kanda ya magharibi kilichopo Tabora, umbali wa karibu Km 450
kutoka Kigoma mjini. Ambapo pia upatikanaji wa damu salama umekuwa
hautoshelezi mahitaji halisi ya Kimkoa yanayokadiriwa kuwa chupa 22000
kwa mwaka”, alisema Kanali Mstaafu Machibya.
Alisema ili kukabliana na tatizo
hilo Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
wadau wengine wa maendeleo uliamua kujenga kituo kidogo cha Damu Salama
katika eneo la Hospitali ya Maweni ujenzi wa kituo hicho ambacho
kikikamilika kitaboresha upatikanaji wa damu ndani ya Mkoa na kuboresha
utoaji wa huduma za afya umeshaanza na utakamilika ndani ya wiki mbili
zijazo.
Katika
maadhimisho hayo Mama Kikwete alizindua mfumo wa kiektronic wa
kuhifadhi kumbukumbu za wachangia damu nchini. Pia alitoa kikombe kwa
mshindi wa kitaifa kwa mwaka 2013/14 cha sisi ni mashujaa tumeokoa
maisha na cheti kwa Shule ya Sekondari ya Bihawana iliyopo mkoani
Dodoma kwa kutoa chupa nyingi za damu kwa mkupuo ukilinganisha na
idadi ya wananchi waliokuwepo na katika ngazi ya mkoa kikombe kidogo
kama hicho kilienda kwa Shule ya Sekondari Kasulu.
Mke
huyo wa Rais pia alitoa cheti kwa mwanaume aliyechangia damu nyingi
kuliko wote nchini kwa mwaka 3013/14 hii ikiwa ni mara 53 katika maisha
yake Emmanuel Essay kutoka mkoa wa Kilimanjaro na kwa upande wa
mwanamke cheti hicho kilienda kwa Restituta Mushi kutoka mkoa wa Mwanza
ambaye amechangia mara 28.
Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Leonard Subi alitambuliwa na mpango wa damu
salama kwa mwaka 2013/2014 na kupewa cheti kutokana na juhudi za ziada
alizozifanya za kufuatilia upatikanaji wa damu katika Hospitali zake,
kwa kushirikiana na mpango wa Taifa wa Damu salama ameweza na
kuhamasisha Halmashauri kutenga bajeti ya kukusanya damu salama na
amefanikisha ujenzi wa kituo kidogo cha kukusanyia damu.
Siku ya wachangia damu Duniani ambayo Kauli mbiu ya mwaka huu ni DAMU SALAMA UHAI WA MAMA ni
ukumbusho wa siku ya kuzaliwa kwa Karl Landsteiner ambaye ndiye
aliyegundua mfumo wa makundi yay a damu A, B na O na alizawadiwa tuzo ya
Nobel kutokana na ugunduzi huo.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Kigoma
0 Comments