MADIWANI KINONDONI WALIA NA MAISHA CLUB


Na Shehe Semtawa

IDARA ya Utamaduni Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam imeagizwa kuchukua hatua za kuuonya uongozi wa Ukumbi wa Buruda wa Maisha Klabu kujiepusha na vitendo vya uhamasishaji wa ngono na kuwadhalilisha wanawake.

Kauli hiyo ilitolewa na Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni jijini jana, walipokuwa wakijadili maendeleo ya wilaya hiyo.

Walisema agizo hilo linatokana na vitendo vinavyofanyika katika ukumbi huo ambako wanawake wanadhalilishwa kutokana na kucheza wakiwa uchi wa mnyama huku wakitiwa chupa za bia kwenye sehemu zao za siri.

Diwani wa Sinza, Renatus Pamba,(Chadema) ambako ndiko kwenye ukumbi huo alisema, mtindo wa uchezaji huo unaitwa bunyelobunyelo, ambao hauendani na maadili ya kitanzania.

“Ni jambo la hatari sana kwani hatujui kimaadili tunawafundisha nini Watanzania pia mama, dada zetu wanadhalilishwa mno kitendo ambacho hakikubaliki kwa viongozi makini kama sisi,”alisema Pamba.

Tatu Maliyaga, alisema ratiba ya wiki inaonesha kuwa siku ya Jumatano inakuwa maalumu kwa wanawake na Alhamisi kwa Mashoga , ambako mashoga wote wa mkoa wa Dar es Salaam hukusanyika katika ukumbi huo na kufanya vitu vichafu wanavyovijua.

“Wakati taifa likipambana na kupunguza ongezeko la maambukizi mapya ya ugonjwa wa ukimwi, tunashangaa wengine kwa makusudi wanaamua kuipotosha jamii,”alisema Maliyaga.

Pamoja na kwamba leseni ya biashara hiyo imetoka ngazi za juu zaidi ya Manispaa, bado Idara ya utamaduni ina nguvu kisheria katika kuzuia uchafu huo, endapo itashindikana, ni vema zikatafutwa njia za kisheria zitakazosaidia kwa kufungwa kabisa klabu hiyo.

Maliyaga, aliongeza kuwa hawako tayari kuona tabia hizo za kifuska  zinazoporomosha maadili ya Watanzania zikiendelea katika wilaya hiyo.


Post a Comment

0 Comments