BONDIA YUSUPH MNYETO ANGIA NGUMI ZA KULIPWA RASMI




Yusuph Mnyeto ‘Super Boy’ ‘Mtoto’ wa Kova aliyepania kufuata nyayo za Rashid Matumla Na Michael Komba NDONDI ni miongoni mwa michezo ambayo imewahi kuitangaza vilivyo Tanzania katika anga ya kimataifa, kama ilivyokuwa kwa riadha. Mabondia ambao waliwahi kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, ni Michael Yombayomba, Habibu Kinyogori, Titus Simba, Emmanuel Mlundwa, Rashid Matumla na wengineo. Soka ambayo ndio mchezo unaopendwa na kupewa kipaumbele zaidi hapa nchini, haujawahi kuiletea Tanzania mafanikio yoyote, zaidi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria. Zaidi ya mafanikio hayo, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars na hata klabu zetu, zimebaki kuwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ katika michuano mbalimbali ya kimataifa. Angalau riadha na ndondi zimefurukuta kwa kutwaa medali katika mashindano makubwa kama michezo ya Olimpiki na Michezo ya Afrika (All Africa Games’. Pamoja na hilo, mchezo wa ndondi bado unaonekana kupewa kisogo na wadau kwa kushindwa kuboresha miundombinu yake kama kumbu za kisasa na mengineyo kama hayo. Hadi sasa, hakuna kumbi za kisasa za mchezo huo hapa nchini ambazo zingesaidia kuwahamasisha vijana wadogo wa kitanzania kujikita katika ndondi. Hatahivyo, bado kila siku ya Mungu vijana wa kitanzania wameonekana ‘kupambana’ kujaribu kuendeleza vipaji vyao kupitia ndondi, baadhi yao wakifanya hivyo bila kupata uangalizi sahihi wa kitaalamu. Mathalani, katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, unaweza kuwakuta vijana wadogo wakiwa wamening’iniza kiroba kilichojaa mchanga juu ya mti, wakijifua waweze kutimiza ndoto zao za kuwa mabondia maarufu hapa nchini na duniani kwa ujumla. Wapo wanaofanya hivyo ili waweze kufikia mafanikio ya mabondia waliopita kama Yombayomba, Simba; lakini wengi wakisikika wakimtaja Rashid Matumla, ambaye ndiye bondia wa miaka ya hivi karibuni kuwahi kutamba hapa nchini na hata katika medani ya kimataifa, akitwaa mikanda lukuki kabla ya kustaafu. Yusuph Mnyeto ‘Super Boy’, ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vya ndondi ambaye ameona ni vyema akakitendea haki kipaji chake hicho. Kijana huyo mwenyeji wa mkoani Tanga, ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi chini ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiwa anapatikana pale Polisi Ufundi, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya ndondi ya Polisi jijini. Na baada ya kudumu katika ndondi za ridhaa kwa muda mrefu kidogo, Mnyeto ameamua kubadili upepo na kuhamia kwenye ndondi za kulipwa. Akizungumzia uamuzi wake wa kuhamia ndondi za kulipwa, Mnyeto anasema kuwa alifanya hivyo kama sehemu ya hatua za maisha yake katika mchezo huo aliodai kuwa anaupenda mno. “Nimekuwa katika ngumi za ridhaa kwa muda mrefu, na sasa nimeamua kuhamia ndondi za kulipwa, nikiamini ninaweza kupata mafanikio makubwa kwani nina usongo wa kulipa sifa Jeshi la Polisi pamoja na nchi yangu kwa kufanya mambo makubwa kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa. “Katika maisha yangu ya ndondi, nimekuwa nikipata sapoti ya hali ya juu kutoka kwa mwajiri wangu na wachezaji wenzangu ambao nao ni askari Polisi… naondoka ngumi za ridhaa kwenda za kulipwa, nataka kurejesha hadhi ya ndondi ndani ya Jeshi la Polisi. “Matarajio yangu ni kufuata nyayo za Haji Matumla ambaye ni askari Polisi, Yombayomba (Michael) na wenginbeo, ikiwezekana hata kuwazidi, naamini hilo linawezekana kama kila kitu kitakwenda kama nilivyopanga.” Aliongeza: “Nataka kufanya kitu tofauti, nashukuru hata rafiki na ndugu zangu, wananisapoti, sitaki kubahatisha, ndio maana nimetafuta kocha mzuri mwenye uzoefu, kama Rashind Matumla, ambaye nashukuru amenipokea na kunikaribisha katika ‘gym’ yake. “Kwangu Rashid Matumla ni mtu muhimu sana, nimekuwa nikimshabikia tangu nilipokuwa mtoto na nilitamani siku moja nije kuwa kama yeye au hata kumzidi. “Kufanya mazoezi katika ‘gym’ yake (Matumla), kunanisisimua sana, ninapoona picha zilizopo katika ukuta wa gym yake akiwa anapigana, akiwa amebeba mikanda mbalimbali ya ubingwa wa Dunia, na hata habari za kwenye magazeti za kumpongeza, ninapata hisia kali sana.” Anasema kuwa kikubwa zaidi, ni kuona bingwa huyo wa zamani wa Dunia wa WBU ambaye alishiriki mara tatu michezo ya Olimpiki, mwaka 1988, 1992 na 1996, akimpa moyo wa kufuata nyayo zake “Kaka Rashid amekuwa akinipa moyo kuwa kutokana na jinsi alivyoniona, ninaweza kuwa bondia mzuri kama yeye au hata kumzidi, lakini kama nitafanya bidii katika mazoezi, kuzingatia nidhamu na miiko ya mchezo huu wa ngumi.” Mnyeto anaelezea hali ya ndondi ilivyo ndani ya Jeshi la Polisi, akisema: “Polisi kuna wachezaji wazuri sana, tatizo ni hamasa, hivyo nimeona ni vyema nikawafungulia njia wenzangu kwani hakuna sababu yoyote ya kutofika mbali katika mchezo huo, maana mwajiri wetu anajali sana michezo si kama katika sekta nyingine.” Kwa upande wa ndondi za ridhaa, anasema kuwa tatizo lililoko huko ni uongozi wa chama husika kutokuwa na mikakati ya kuuendeleza mchezo huo. “Katika ngumi za ridhaa hapa nchini, tatizo ni uongozi, pale kuna mtu mmoja tu, Mashaga (Makore), jamaa anajitahidi sana kupambana, kama angepata msaada, basi mambo yangekuwa mazuri zaidi,” anasema. Na sasa Mnyeto ni ‘hakuna kulala’, kila baada ya kumaliza majukumu yake ya kikazi, hugeukia mazoezi ya ndondi katika gym ya Matumla na wakati mwingine kwenda kwenye klabu nyingine za mazoezi. Katika mazoezi yake hayo, wakati fulani amekuwa pia akinolewa na Haruna Andrew ‘Ndimu Mkata Shombo’ ambaye naye ni bondia. Matarajio yake kwa siku chache zijazo ni kupata pambano la kujipima nguvu dhidi ya bondia atakayejitokeza kukabiliana naye. “Kabla ya kupata pambano, niliona ni vyema nikajifua kwanza kwani kuna kipindi nilisimama kufanya mazoezi, hivyo lazima niwe fiti kabla ya kupanda ulingoni,” anasema. Anasema kuwa matarajio yake mapema mwezi ujao atakuwa fiti tayari kuonyesha ubabe na bondia yeyote atakayekubali kupigana naye. Hata hivyo, alisema kuwa katika kufanikisha azma yake hiyo, hatasita kuwa bega kwa bega na mwajiri wake ambaye ni Jeshi la Polisi kuhakikisha kipaji chake hicho hakiathiri majukumu yake ambayo ndiyo yanayomwezesha kufanikisha baadai ya mambo kuelekea mkakati wake wa kuwa bondia hatari hapa nchini. “Pamoja na haya yote, ninaiheshimu sana kazi yangu kwani ndiyo inayonifanya niwe na jeuri ya kutamba kutaka kufuata nyayo za akina Matumla, bila Jeshi la Polisi, nisingekuwa kama nilivyo sasa,” anasema Mnyeto. Bondia Yusuph Mnyeto, alizaliwa Februari 20, mwaka 1982 katika eneo la Ngamiani, jijini Tanga, akiwa ni mtoto w asaba katika familia ya watoto saba wa Mzee Mnyeto. Alianza masomo yake katika Shule ya Msambweni, jijini humo na baadaye kujiunga na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mwaka 1995.Mnyeto ambaye kwa sasa hajaona, lakini akiwa na mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa muda si mrefu, alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 2000 na hadi sasa analitumikia jeshi hilo, kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Pamoja na kulitumikia Jeshi la Polisi na kuendeleza kipoaji chake cha ndondi, Mnyeto anekuwa akitenga muda wake kwa ajilki ya kujiendeleza kimasomo. “Kama unavyofahamu, elimu ni kila kitu na haina mwisho, nashukuru mwajiri wangu (Jeshi la Polisi), hana kikwazo na mtu anayetaka kujiendeleza kimasomo, kwa kweli ninashukuru sana kwa hilo,” anasema Mnyeto. Juu ya mkakati wake wa kuendelea na masomo, anasema: “Ndondi inaonekana kama ni mchezo wa akina ‘Kayumba’ (watu wasio wasomi), tusikubali ujinga, mabondia twendeni shule.” Kuhusiana na malengo yake baada ya kuanza kupata mafanikio katika ndondi, anasema amepania kufungua klabu yake ya mazoezi ya ndondi (gym) ambayo itakuwa katika ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana chipukizi kujinoa waweze kutimiza ndoto zao. “Lengo langu ni kufungua ‘gym’ ambayo itakuwa na hadhi ya kimataifa, kama ilivyo Azam Complex ya klabu ya soka ya Azam. Juu ya kilio cha mabondia wengi kutaka wadhamini kujitokeza katika mchezo huo, Mnyeto anaasa: “Tusitegemee zaidi wadhamini, tujitegemee, tusipigane kuganga njaa, kwani tunadhalilishwa kwa kutojitambua, maana ukipigwa unajirudisha nyuma na umaarufu wako unapotea.”  tunamtakia kila la kheri Yusuph Mnyeto kuelekea jitihada zake za kuwa bondia wa kulipwa mwenye mafanikio hapa nchini, tukiamini hilo linawezekana iwapo atajipanga hasa na kuzingatia miiko ya mchezo huo.

Post a Comment

0 Comments