ALLY CHOKI ALIZWA SAA YA DOLA 300 YA SILVERA


 Mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi Extra Bongo 'Next Level' 'Kamarade' 'wazee wa Kimbembe' Ally Choki alijikuta akimwaga machozi baada ya watu wanaodhaniwa kuwa vibaka kujipenyeza wakati wa uzinduzi wa albamu ya 'Mtenda Akitendewa' iliyozinduliwa Februari 22 mwaka huu na kumuibia saa ya silva yenye thamani ya dola 300 sawa na sh.500,000.
Extra Bongo ilizindua albamu hiyo ndani ya Ukumbi wa Dar Live Mbagala jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki na wadau wa muziki wa dansi ambapo Choki aliingia ukumbini akiwa ndani ya gari la kubeba wagonjwa 'Ambulance' na kulakiwa juu kwa juu.
Choki, alieleza, tukio la kuibiwa lilimkuta wakati akishuka kwenye ambulance ambapo ndani ya kundi la mashabiki waliompokea kulikuwepo na vibaka waliofanikwa kumvua saa hiyo pasipo yeye kujitambua.
"Kwa kweli saa yangu inaniuma sana nililetewa zawadi na rafiki yangu kutoka Qatar lakini ndo hivyo vibaka wameniingiza mjini alisema Choki kwa masikitiko na kuongeza.
"Wakati nimepanda jukwaani ndiyo nikashtukia nimelambwa saa, bahati nzuri simu na vitu vyangu vingine vya thamani nilikuwa nimeviacha kwa mlinzi wangu vinginevyo hali maumivu yangekuwa makali zaidi ya hivi.
Tukio la Choki kuibiwa linakumbusha tukio jingine lililowahi kutokea miaka kadhaa nyuma kwa aliyekuwa rapa wa bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) Papii Kocha 'Mtoto wa Mfalme' kuporwa cheni na vibaka akiwa jukwaani wakati wa uzinduzi wa moja ya albamu za bendi hiyo katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Aidha Choki alisema atatoa zawadi ya sh.300,000 kwa mtu yoyote atakayeweza kufanikisha kupatikana kwa saa hiyo huku akitaka aliyeiba kumrejeshea kiroho safi na atampatia kiasi hicho cha fedha pasipo kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

"Nimeamua kutoa zawadi kwa atakayewezesha niipate saa yangu au kwa aliyechukua kuirudisha kwangu, hii ni sababu nilikuwa naipenda sana alieleza.

Post a Comment

0 Comments