Babi ang'ara Malaysia, licha timu yake kulala 1-0



Abdi Kassim (wa kwanza kulia mbele) akiwa na kikosi cha timu yake ya UiTM
 KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Malaysia, Abdi Kassim 'Babi' leo amechaguliwa kuwa Nyota wa Mchezo (Man of the Match) baada ya kung'ara katika pambano la Ligi Kuu ya nchi hiyo, licha ya timu yake ya UiTM kulazwa bao 1-0 ugenini.
UiTM iliifuata Palau Pinang kwenye uwanja wao wa Bandaraya, mjini Penang na kukumbana na kichapo hicho kinachoifanya timu hiyo kusaliwa na pointi zao nne ikijikusanyia pointi nne kutokana na mechi tatu ilizocheza mpaka sasa katika ligi.
Hata hivyo kiwango alichokionyesha mchezaji, kilimfanya kuchaguliwa nyota pambano hilo, kitu ambacho mwenyewe amekielezea kama faraja kubwa kwake tangu atue nchini humo kucheza soka la kulipwa akitokea KMKM aliyoichezea kwa kipindi kifupi.
Akizungumza na MICHARAZO, Babi alisema pambano lao la leo lilikuwa kali na lenye ushindani kutokana na wenyeji kuwakamia, lakini alionyesha uwezo mkubwa na mwishoni pamoja na timu yao kulala alitangazwa Mchezaji Bora.
"Licha ya timu yetu kupoteza pambano letu la leo ugenini, lakini nashukuru nimeweza kung'ara na kuchaguliwa mchezaji bora kwa kiwango cha soka nilichoonyesha, nimefarijika na ninapigana zaidi ili kufanya vizuri na kuisaidia timu yangu,' alisema Babi.
Babi alisema timu yake itashuka tena dimbani siku ya Jumatatu kuikaribisha timu ya PDRM katika pambano jingine la ligi hiyo inayozidi kushika kasi tangi ilipoanza Januari 24.

Post a Comment

0 Comments