Mke
wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi,(kulia)
pamoja na marafiki wakiomba dua leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) katika
Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere dakika chache kabla na Dkt. Mvungi
hajasafishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Kushoto ni
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia. Dkt. Mvungi alivamiwa na
kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam usiku wa
kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.
Dkt.
Mugisha Clement Mazoko wa Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) (kushoto),
Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid (mwenye tai) na
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Bw. James Mbatia (wa pili kulia) pamoja na
ndugu na jamaa wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo
Mvungi wakiangalia wakati Mjumbe huyo akipandishwa ndani ya ndege
kusafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Dkt. Mvungi
alivamiwa na kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es
Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.
*************************************************
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Mjumbe
wake Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Kitengo cha
Mifupa Muhimbili (MOI) amesafirishwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) saa
5:45 asubuhi kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu
zaidi.
Akiwa nchini Afrika Kusini, Dkt. Mvungi atapata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg.
Itakumbukwa
kuwa Dkt. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa
kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013. Tukio hilo la uvamizi
linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Tangu
siku alipojeruhiwa, Dkt. Mvungi alikuwa akipata matibabu katika Kitengo
cha Mifupa Muhimbili (MOI). Hata hivyo, Madaktari waliokuwa wakimtibu
MOI, walishauri afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi.
Dkt.
Mvungi ameondoka na ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink
na ameambatana na Dkt. Mugisha Clement Mazoko kutoka MOI; Muuguzi Bi.
Juliana Moshi; na mtoto wa kaka yake Bw. Deogratias Mwarabu. Serikali
inagharamia gharama zote za matibabu ya Dkt. Mvungi.
Tume
inawaomba wananchi wote waendelee kumuombea kwa Mungu Dkt. Mvungi ili
aweze kurejea katika hali yake ya kawaida na hatimaye kuendelea majukumu
yake.
0 Comments