WAANDISHI WA HABARI WAPIGWA 'STOP' KURIPOTI UCHAGUZI WA TFF



Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) Juma Pinto (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari nje ya Ukumbi wa Mikutano NSSF  'Water Front', mahala unapofanyika Uchaguzi mkuu wa Rais na viongozi wa Soka wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF).

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Waandishi wa Habari  wamezuiwa kuripoti habari za uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa NSSF Water Front.
Baada ya waandishi kuzuiwa, askari waliokuwa wakilinda usalama katika uchaguzi huo waliwataka waandishi kuondoka na kukaa mbali na ukumbi huo huku  Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto, akiwataka waandishi kususia kuandika na kuripoti matokeo ya uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kutoandika taarifa za TFF.
Pinto alisema kitendo cha TFF kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni, kuwazuia waandishi kuripoti habari hizo ni cha udhalilishaji kwa kuwa waandishi ndio waliokuwa mstari wa mbele kuandika taarifa za uchaguzi huo tangu mchakato wake ulipoanza Februari mwaka huu.
Alisema mbali na kutoruhusiwa kuripoti uchaguzi huo, Mbwezeleni ametoa kauli ambazo si za kiungwana na kusahau kuwa waandishi ndio waliokuwa mstari wa mbele kuwajuza Watanzania kuhusu uchaguzi huo kwa faida ya maendeleo ya soka la Tanzania.

 Kufuatia hali hiyo, iliwalazimu waandishi kukaa nje ya ukumbi huku wakiuliza kwa wajumbe kitu gani kinachoendelea ndani ya ukumbi.

Post a Comment

0 Comments