KUTUPIANA MPIRA HUKU HAKUIJENGI SANAA YETU

MSANII SHILOLE AKIWA JUKWAANI (PICHA ZOTE NA MPEKUZIBLOG)


MWISHONI mwa wiki iliyopita, msanii wa muziki wa kizazi kipya, akiimba miondoko ya mduara, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, aliripotiwa kukiuka maadili ya Kitanzania wakati akitumbuiza katika tamasha la Serengeti Fiesta 2013, mkoani Iringa.

Kutokana na tukio hilo, ambalo Shilole inadaiwa alinengua jukwaani akiwa kavaa nusu uchi, Shirikisho la Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, chini ya Mwenyekiti wake, Kimela Billa, lilielezea kukerwa na hali hiyo, hivyo kuliagiza Shirikisho la Muziki Tanzania kuchukua hatua kwa msanii huyo.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, vitendo kama hivyo vilivyofanywa na Shilole, havipaswi kufumbiwa macho, hivyo Shirikisho hilo la Muziki linapaswa kuchukua hatua kama lilivyofanya Shirikisho la Filamu mwaka jana, kwa wasanii Wema Sepetu na Aunt Ezekiel, ambao nao walifanya vitendo kama hivyo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Rais wa Shirikisho la Muziki, Ado November, naye akakaririwa akidai hawana sauti ya kusema wakasikika juu ya jambo lolote linalohusu muziki hivi sasa.

November aliongeza kuwa, hata kama wakisema, hakuna atakayewasikia, kwa sababu Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), halijawapa makali ya kukata.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba, makali hayo ni yapi!

Ninyi ndiyo shirikisho ambalo linafanya kazi na wanamuziki, sasa iweje mdai ni vibogoyo? Hapa kuna maswali lukuki na sintofahamu.

Na kama ni kweli Basata halijawapa makali, basi kuna matatizo ya kiutendaji hususan katika uundaji wa mashirikisho hayo.

Kama ndivyo, Basata kama ilivyosimamia uundwaji wa vyombo hivyo, basi inapaswa kukaa chini na kutafakari upya malengo na utendaji wa mashirikisho hayo.

Akizungumzia zaidi kuhusiana na kukosa ubavu, November alisema, hivi sasa wao kama Shirikisho hawana meno ya kumwadhibu au kutoa onyo kwa msanii yeyote huku akilitupia mzigo Basata kumchukulia hatua Shilole.

“Hivi sasa sisi Shirikisho hatuna meno wala nguvu, kwa sababu hatutoi vibali, hivyo Basata wanapaswa watoe kauli yao iliyo thabiti katika jambo hili la fedheha,” anasema November na kuongeza.

Basata ndiyo wanaotoa vibali na kupelekewa muhtasari namna tamasha litakavyofanyika, pamoja na kupewa majina ya wasanii watakaopanda jukwaani, hivyo kama msanii alikiuka maadili katika Mkoa mmoja, wampe onyo ili asifanye hivyo kwingine ama aadhibiwe ipasavyo iwe mfano kwa wengine.

November, aliwaomba wananchi popote walipo, wawadharau wasanii wote ambao wamekuwa wakiona sifa kuidhalilisha jamii kwa kuanika maungo yao mbele ya kadamnasi.

Safu hii inasema kwamba, katika hali yoyote ile, katika hili hakuna manufaa ya kutupiana mpira kwa manufaa ya jamii yetu ya Kitanzania.

Tunaamini, kwa busara tu, Shirikisho la Muziki lina nafasi ya kukemea hili kama jinsi walivyofanya wenzao wa Filamu (TAFF).

Inakumbukwa kwamba, TAFF waliitisha mkutano na wandishi wa habari na wasanii hao wakaomba msamaha kwa Watanzania, kutokana na vitendo vya aibu walivyovifanya.

Hivyo kitendo cha November kudai kuwa wako kimaonyesho zaidi na si kivitendo, ni cha aibu na kinachoibua maswali, kuna haja gani kuwepo kwa viongozi hao ili hali wanajijua hawana la kufanya?

Wito kwetu kwa pande zote, zikae chini na kuangalia namna ya kutekeleza majukumu yao na si kutupiana mpira, kwani hakujengi, bali kubomoa maadili ya jamii yetu.
NB:MAKALA HII IMECHAPISHWA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAILA LEO TOLEO NO.3213 SAFU YA BUSATI INAYOTOKA KILA SIKU YA IJUMAA.

Post a Comment

0 Comments