KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) WAKUTANA


Amir Mhando

 
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana Dar es Salaam Ijumaa Septemba 27, 2013 kujadili masuala mbalimbali chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Pinto.
 
(A) MKUTANO WA KATIBA/UCHAGUZI MKUU
 
Kikao kilikubaliana sekretarieti ya TASWA ishirikiane na Kamati ya Katiba ya TASWA inayoongozwa na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti, Frank Sanga kuhakikisha mchakato wa Rasimu ya Katiba mpya ya chama hicho unaenda vizuri.
 
Kamati  hiyo ya katiba itasimamia mchakato huo na ihakikishe kabla ya Desemba 15 mwaka huu, rasimu hiyo iwe tayari na ikabidhiwe kwa Kamati ya Utendaji ya TASWA, ambayo itaiwasilisha kwenye Mkutano Mkuu wa Katiba wa chama utakaofanyika Desemba 21 mwaka huu, mahali patakapotangazwa.
 
Hata hivyo Kamati ya Utendaji imeiagiza sekretarieti ya TASWA kujipanga vizuri ili kuhakikisha mkutano wa kujadili Katiba unafanyika nje ya Dar es Salaam kuwezesha wajumbe wawe watulivu zaidi na kufanya uamuzi sahihi kuhusiana na katiba yao.
 
Pia kikao hicho kimepanga Uchaguzi Mkuu wa TASWA ufanyike Januari 18 mwakani jijini Dar es Salaam. Utaratibu zaidi kuhusiana na uchaguzi huo utatangazwa, lakini si dhambi wala si nongwa kwa wanaotaka kuingia madarakani wakianza kutangaza nia mapema. Pia wanachama wametakiwa kulipia ada zao kabla ya Novemba 30 mwaka huu.
 
(B)  TUZO ZA WANAMICHEZO BORA
Chama chetu kila mwaka kimekuwa kikiendesha tuzo za Wanamichezo Bora, lakini mwaka huu tumechelewa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo baadhi ya wadhamini waliokubali awali kutusaidia kushindwa kutekeleza ahadi zao.
 
Hata hivyo suala hilo sasa  limepatiwa ufumbuzi na Jumatano Oktoba 2, 2013, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto atafanya mkutano na waandishi wa habari kwenye mgahawa wa City Sports Lounge, Dar es Salaam saa tano asubuhi kuzungumzia suala la tuzo pamoja na kutangaza tarehe ya kufanyika kwake. Atakuwepo pia Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Haji Manara.
 
(C)  MAFUNZO
Kama mnavyofahamu TASWA na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameingia ushirikiano ya kuendesha mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo nchini.

Kuna muelekeo mzuri kuhusiana na jambo hilo, ambapo vyombo hivyo vinaendelea na mazungumzo na wadhamini zaidi kwa nia ya kuyafanya mafunzo hayo yawe bora na tayari wapo waliojitolea kutusaidia ingawa ingawa si kwa bajeti yote.
 
(D)      Uchaguzi Mkuu wa TFF
Kikao kilijadili kwa kina suala la uchaguzi wa TFF na kuweka jambo hilo kiporo kwanza na kufanyia kazi baadhi ya changamoto, hadi Jumanne Oktoba 1 mwaka huu, ambapo kikao kingine cha Kamati ya Utendaji kitafanyika.
 
(E)       UANACHAM WA AIPS
TASWA ni mwanachama hai wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS) chenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi na kila mwaka tumekuwa tukishiriki kwenye mikutano, lakini wanachama wetu asilimia kubwa hawana kadi za AIPS kwa vile si wanachama.

Faida za kadi hizo unaweza kutumia viwanja vya michezo mbalimbali duniani ambako kuna vyama vya waandishi wa habari za michezo.

Naomba kuwajulisha kuwa utaratibu wa kupata kadi za AIPS kwa mwaka 2014 tayari umeanza, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake aombe kwa njia ya mtandao huu:http://www.aipsmedia.com/index.php?page=getcard.
Ukishakubaliwa fomu yako utaelekezwa uwasiliane na TASWA, ambapo utapewa utaratibu wa malipo ambayo ni dola za Marekani kumi (10) tu, ambapo gharama za utumaji wa ada hizo kwa fedha za kigeni kabla ya Novemba mosi mwaka huu chama kitaingia.

Lakini baada ya muda huo kupita, wale ambao watachelewa kujaza fomu bado watakuwa nayo nafasi ya kupata kadi hizo, ila watalazimika kuingia gharama za kutuma fedha za kigeni nje, ambazo chama hakitabeba tena jukumu hilo.
 
Nawasilisha.
 
Amir Mhando
 
Katibu Mkuu TASWA
29/09/2013

Post a Comment

0 Comments