MAMA SALMA KIKWETE NA WAKE WA MARAIS WALIOKUWA KWENYE MKUTANO WA SMART PARTNERSHIP WATEMBELEA MAONESHO.



 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongozana na Mheshimiwa Inagosi Bulo kutoka DRC (kushoto) na Inkhosikati Lambikiza wa Swaziland na Mama Charlotte Scott wa Zambia wakiwa nje ya banda la Zanzibar mara baada ya kutembelea banda hilo jana.
 Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Maendeleo Mama Salma Kikwete akiangalia bidhaa mbalimbali za aina ya shanga zilizokuwa zikionyeshwa kwenye banda la SIDO wakati walipotembelea maonesho hayo.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na wageni wake wakiangalia mashine ya kutengeneza nguo aina ya vikoi kwenye banda la SIDO wakati walipotembelea banda hilo.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifuatana na Waziri Inagosi Bulo kutoka DRC (kushoto) na Inkhosikati Lambikiza wa Swaziland (kulia) wakiangalia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kutoka kwenye mnazi kama zilivyokuwa zikionyeshwa na akina mama kwenye banda la WIPE.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifuatana na wageni wake wakitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho wakiongozwa na Naibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Gregory Teu.
****************************

*Mama Kikwete awataka watanzania kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini

Na Anna Nkinda – Maelezo
Watanzania wametakiwa kujifunza kuthamini  vitu vya kwao na kuona kuwa ni bora zaidi kwa kufanya hivyo hata wageni watavipenda  kwani bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi  hazitapandishwa thamani na watu kutoka nje. 

Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kutembelea maonyesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika  uwanja wa Mwalimu Nyerere uliopo barabara ya Kilwa wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete aliambatana  na Mke  wa Mfalme Mswati  wa Swaziland Inkhosikati  Lambikiza, Mke wa Makamu wa Rais wa Zambia Mama Charlotte Scott na  Mwakilishi wa Mke wa Rais Joseph Kabila wa Jamuhuri ya watu wa Congo ambaye ni Waziri wa Jinsia, Watoto na Familia Inagosi Bulo.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa walitembelea maonyesho hayo  ili  kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa ndani na nje ya nchi  kuanzia ngazi ya juu hadi  chini. 

“Tumeona bidhaa za aina mbalimbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi na jinsi watu wanavyoweza kubadilishana uzoefu wa biashara hakika kadri siku zinavyozidi  kwenda kuna maboresho makubwa juu ya utengenezaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini”, alisema Mama Kikwete.

Aliwashukuru wageni alioambatana nao kwa kuzipenda bidhaa zilizopo kwenye mabada ya watanzania na kuwaomba wananchi kutoka  maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam kutembelea  maonyesho hayo kwani kuona ni kujifunza.

Pia  aliwapongeza na kuwashukuru wanawake kwa kazi kubwa wanazozifanya za kuzalisha bidhaa na kufanya biashara mbalimbali ambazo zimewasaidia  kujiletea maendeleo yao na jamii inayowazunguka.

Post a Comment

0 Comments