Na Elizabeth John
FILAMU ya aliyekuwa nguli wa
filamu nchini, Marehemu Steven Kanumba, inayojulikana kwa jina la ‘Love
and Power’ inatarajiwa kuzinduliwa rasmi keshokutwa katika viwanja vya Leaders,
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Marehemu Steven Kanumba |
Akizungumza jijini Dar es
Salaam, mdogo wa marehemu Kanumba ambaye pia ni kiongozi wa ofisi
yake ya ‘Kanumba The Great’ iliyopo Sinza, Seth Bosco alisema wameamua
kuizundua siku hiyo kutokana na kuwa na kumbukumbu ya kutimiza mwaka moja tangu
kilipotokea kifo chake.
Alisema zaidi ya waigizaji 10
kutoka Ghana
wanatarajia kuwepo siku hiyo ikiwa ni pamoja na rafiki wa marehemu,
ambaye ni muigizaji maarufu barani Afrika, Mnigeria, Ramsey Noah.
“Ramsey amethibitisha kuwepo
katika uzinduzi huu na anatarajia kuingia nchini kesho (leo),” alisema Bosco.
Akizungumzia ratiba ya siku
hiyo ya uzinduzi alisema, itaanzianyumbani kwa marehemu, baada ya hapo wataelekea makaburini na baadae Leaders kwa ajili ya uzinduzi huo.
Alisema wapenzi na mashabiki wa filamu za Kanumba wanatakiwa kufika asubuhi nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya ibada ya kumsalia itakayoanza saa nne asubuhi na kuisha saa tano.
Alisema mara baada ya ibada hiyo ndugu, jamaa, marafiki, waigizaji pamoja na mashabiki wake watakula chakula cha pamoja kisha kuelekea makaburini.
Alisema bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta ndio itahusika siku hiyo kwa upande wa burudani, kisha uzinduzi rasmi utafanyika huku kopi za filamu hiyo zikiuzwa hapopapo.
Marehemu Kanumba alifikwa na umauti Aprili 7 mwaka jana nyumbani kwake Sinza Vatcan, huku kifo chake kikihusishwa na msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
0 Comments