MWANAMITINDO
mahiri wa kimataifa ambae pia aliwahi kuwa Miss Tanzania 2001, Millen
Happiness Magese amewagusa wakazi wa Mtwara kufuatia ziara yake ya
kimafanikio aliyoifanya mkoani humo na kukabidhi misaada mbalimbali.
Millen
ambae kwa sasa anaishi nchini Marekani akijishughulisha na fani ya
mitindo akiwa Mtwara alipokelewa na viongozi mbalimbali wakiwamo Mkuu wa
Wilaya ya Mtwara; Mhe. Willman Ndile, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara; Mhe.
Simbakali na Mbunge wa Mtwara mjini; Mhe. Hasnain Murji.
Millen
alitoa fedha taslim kiasi cha shilingi milioni 15 ambapo milioni 10
ilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ya Mjimwema baada ya
kutembelea shule hiyo na kuguswa na hali ya mazingira magumu aliyoyakuta
katika shule hiyo iliyopo kata ya Magengeni.
Millen
awali alikuwa ametaka kupeleka msaada wake huo katika shule ya msingi
ya LiLilungu iliyopo Mtwara mjini lakini alijikuta akimwaga milioni kumi
kwa shule ya Mjimwema na kuongeza milioni tano kwa ajili ya madawati ya
shule ya Lililungu kwani awali alikuwa ameahidi kutoa milioni kumi.
Shule
hiyo yenye madarasa mawili yaliyojengwa kwa udongo ambapo wanafunzi
wakiwa ni wengi huku wengi wao wakiwa hawana viatu na sare zao za shule
zikiwa zimechakaa.
Akizungumza
shuleni hapo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Ndile, Millen alisema
kuwa akiwa kama mwanamitindo ameguswa na hali mbaya ya mazingira ya
shuleni hapo hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi wanasomea katika shule ya
udongo huku wakiwa na mazingira duni ya kufundishia.
Aliongeza
na kusema, "Mwaka 2001/2002 nilitembelea mkoa wa mtwara ambao ulinigusa
sana kwenye swala zima la elimu haswa mazingira ambayo yanamfanya mtoto
akae chini. Na nikaahidi siku moja mungu akijalia nitarudi Mtwara na
nimesikitika ni miaka 12 sasa bado watoto wanakaa chini nikaone nirudi
kutimiza ahadi na kutoa hamasa kwenye swala hili la elimu Mkoani
mtwara”; mbali na milioni kumi na tano pia aliahidi kuwatafutia sare za
shule wanafunzi hao jozi mbili kila mmoja na pia alikubali kuwa mlezi wa
shule hiyo.
Pia
alipata fursa ya kukaa na wajasiriamali walioandaliwa semina na mkuu wa
wilaya pamoja na mbunge wa Mtwara mjini kujadili mbinu za kuwaongezea
kipato na kwa kuanzania milioni sita iliyopatikana iligawanywa kwa
wajasiriamali kulingana na vikundi ili wao watengeneze madawati kwa
ajili ya watoto wao, ambapo milioni tano ilitolewa na Millen Foundation
na milioni moja ilitolewa na Mhe. Murji
Baada
ya kuzungumzia ahadi yake hiyo Millen aliwahamasisha wadau wengine
aliiongozana nao kuchangia mchango wa shule hiyo akiwamo Mbunge wa
Mtwara mjini Murji ambae aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili
ya kufanikisha ujenzi zaidi wa shule hiyo na shilingi milioni moja kwa
ajili ya madawati.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara; Mhe Ndile pamoja na Mhe. Murji waliwataka
wananchi kuhamasika zaidi kwa kuunga mkono harakati za Millen katika
kuimarisha elimu mkoani humo kwa kuwa ameonesha mfano mzuri akiwa kama
mwanamitindo.
0 Comments