Amesema Serikali ilianza utekelezaji wa mradi wa reli ya SGR mwaka 2017 huku mwaka 2019 ikianza mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Julius Nyerere, miradi ambayo awali ilipingwa na baadhi ya watu waliodai kuwa isingekuwa na manufaa kwa taifa.
Mwanjala amesema, kwa sasa wananchi wanaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa takribani saa tatu kupitia reli hiyo ya kisasa, jambo ambalo limeongeza ufanisi wa usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Ameeleza kuwa mafanikio ya uendeshaji wa SGR yanategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa umeme kutoka JNHPP, akisisitiza kuwa miradi hiyo miwili inategemeana.

“Ukizungumzia mradi wa SGR huwezi kuacha kuuzungumzia mradi wa JNHPP kwa sababu ndio unaotupa umeme wa kuendesha treni,” amesema.
Aidha amesema kumekuwa na dhana miongoni mwa baadhi ya wananchi kuwa treni za umeme zinaweza kuathiriwa na changamoto za kukatika kwa umeme kama ilivyo kwa matumizi ya majumbani, lakini akafafanua kuwa mfumo wa umeme unaotumika kuendesha SGR ni maalumu.
“Tunapata umeme maalumu kutoka JNHPP na hatushare umeme huo na matumizi ya kawaida ya majumbani. Lengo la mradi wa JNHPP ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha, himilivu na hata wa kuuza nje ya nchi,” amesema Mwanjala.
Kwa mujibu wa Mwanjala, matumizi ya umeme katika uendeshaji wa SGR yanaifanya TRC kutokuwa na sababu ya kuongeza nauli kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia.
“Hatuna sababu ya kupandisha bei au nauli kwa sababu mafuta yamepanda bei, kwa kuwa sisi tunatumia umeme kutoka JNHPP,” amesema Mwanjala.
Katika hatua nyingine, amesema huduma ya SGR imeendelea kuvutia makundi mbalimbali ya watu kutokana na ubora, kasi na ustaarabu wa usafiri huo.
Ametaja baadhi ya wanaotumia huduma hiyo kuwa ni wanadiplomasia, viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, wafanyabiashara pamoja na wanafunzi.
Kutokana na ongezeko la mahitaji ya usafiri huo, amesema TRC imeongeza safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka safari mbili hadi nne ili kuhudumia idadi kubwa zaidi ya abiria.


0 Comments