Kapteni
wa mchezo wa squash wa klabu ya Gymkhana Akil Hirji (katikati)
akikabidhi zawadi kwa Mkrugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Anthony Grant
(wapili kushoto) kama ishara ya kutambua jitihada za kukarabati viwanja
viwili vya mchezo wa squash mwishoni mwa wiki. (Na Mpiga Picha Wetu)
Mkrugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Anthony Grant (katikati)
na Mwenyekiti Msaidizi wa Klabu ya Gymkhana William Chiume (wapili kulia)
wakikata utepe ulikuzindua viwanja viwili vya mchezo wa Squash vilivyokarabatiwa
na benki ya Exim.
DAR ES SALAAM, Tanzania
KATIKA jitihada zake za kusaidia maendeleo ya michezo
nchini, Benki ya Exim Tanzania, imeipiga jeki Klabu ya Gymkhana ya jijini Dar
es Salaam kwa kuikarabatia viwanja vyake viwili vya mchezo wa Skwashi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika hafla ya ufunguzi wa
viwanja hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Anthony Grant alisema
mchango wa benki yake unatokana na kutambua umuhimu wa michezo katika maisha ya
kila siku na kwamba anaamini utasaidia kuendeleza mchezo huo.
“Benki ya Exim tumeamua kushirikiana na Klabu ya Gymkhana
kukarabati viwanja viwili vya skwashi ili kujenga mazingira mazuri ya uchezaji
wa mchezo huo kwa wachezaji. Tunapongeza dhamira ya kitaifa ya Gymkhana, hasa
jitihada zake za kujenga uelewa kwa vijana katika michezo,” alisema Grant.
Grant alibainisha kuwa uwekezaji katika michezo ni suala
muhimu kama nchi inahitaji kupata mabalozi wazuri wa kuliwakilisha taifa nje ya
mipaka na ndiyo maana benki yake imeamua kusaidia ukarabati wa viwanja hivyo,
huku akiyataka makampuni mengine kuiga mfano wa Exim katika uwekezaji.
Kwa upande wake, nahodha wa mchezo wa skwashi wa Klabu ya
Gymkhana, Akil Hirji, alisema kuwa ukarabati wa viwanja hivyo ni msaada mkubwa
utakaoinua maendeleo ya mchezo huo na kusema kuwa klabu itatumia vizuri
miundombinu hiyo iliyoboreshwa.
“Naishukuru Exim kwa msaada wao na nina imani utakuza
maendeleo ya skwashi nchini. Kwa viwanja hivi vya kisasa, wachezaji watakuwa katika
nafasi nzuri ya kushindana kitaifa na kimataifa,” alisema Hirji na kuongeza
Gymkhana imeandaa mashindano ya uzinduzi wa viwanja hivyo yatakayohusisha
wachezaji 30.
0 Comments