Na Veronica Kazimoto – MAELEZODar es Salaam
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imetoa tamko la
kuwataka watendaji wa Serikali, Mahakama, vyombo vya habari na taasisi nyingine
zote kuacha kuzungumzia suala la Uteuzi wa Majaji wa mahakama kuu kama
lilivyowasilishwa Bungeni wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Katiba na
Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa kamati
hiyo Brigedia Jenerali . Mstaafu Hassan Ngwilizi (Mb) amesema suala hilo liko
mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo inaendelea na
uchunguzi hivyo haitarajiwi taasisi nyingine, nje ya Bunge kulizungumzia suala
hili kwa kuwa linajadiliwa na Kamati ya Bunge.
“Kamati imeamua kutoa tamko hili kwa madhumuni ya
kuhakikisha kuwa uvunjifu wa kanuni na taratibu tulizojiwekea kwa mujibu wa
Katiba na Sheria nyingine za nchi kutoendelea kuvunjwa”, amesema Ngwilizi.
Ngwilizi amenukuu Ibara ya 100 ya katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, inayosema kuwa kutakuwa na Uhuru wa mawazo, majadiliano
na utaratibu Katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo
chochote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, au katika mahakama au mahali
penginepo nje ya Bunge.
“Uhuru wa utaratibu unaohifadhiwa na ibara hiyo ya Katiba
umelipa Bunge mamlaka ya kujiwekea utaratibu wa kushughulikia masuala yake
katika Kanuni za Kudumu za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya 89 (1) ya Katiba”,
amesisitiza Ngwilizi.
Kutolewa kwa tamko hilo na kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kunatokana na mwongozo ulioombwa na Gosbert Blandes (Mb)
wakati wa Hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Katiba na
Sheria, Mhe. Tundu Lissu mbunge wa Singida Mashariki.
Katika maelezo yake, Mhe. Blandes alinukuu ukurasa wa 9 aya
ya 2 katika Hotuba hiyo iliyosomeka kuwa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Aya hiyo iliendelea kusema kuwa inaelekea watu hao hupewa
ujaji kama zawadi ili kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo
yameboreshwa na matokeao yake ni kuwa na majaji ambao wamechoka na hawawezi au
hawajui namna ya kufanya kazi ya jaji wa mahakama kuu.
Aidha Blandes alisema msemaji wa kambi ya upinzani
ameingilia mhimili mwingine wa Mahakama ambao hauna nafasi ya kuja kujitetea
ndani ya Bunge na maneno hayo yanalenga kuwadhalilisha Waheshimiwa Majaji
kwamba hawana uwezo, wamechoka, na hawajui namna ya kufanya kazi.
Kufuatia maneno hayo Mwenyekiti wa kikao hicho Jenista
Mhagama (Mb), alitoa mwongozo wake kwa kuiagiza Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge ili ipitie mwenendo wa shughuli yote ya siku hiyo kama
inavyoonekena katika taarifa rasmi za bunge (Hansard) na kulishauri Bunge zima
kwa ujumla wake hatma ya kufanya katika jambo hilo.
0 Comments