BALOZI wa Tanzania Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe amewapongeza wanamichezo wetu walioiwakilisha nchi katika Olimpiki kwa nidhamu ya hali ya juu na kuwataka wasivunjike moyo kwani sio sisi tu tuliokosa medali.
“Wanamichezo wetu wameonesha tabia bora kinyume na watu wa nchi nyingine waliofanya mambo ya aibu sana. Lazima tuwapongeze kwa kufikia viwango na kuibeba bendera ya Tanzania,”alisema. Akiongea katika tafrija ndogo kuwaaga wanamichezo saba, maofisa na makocha wao, Balozi Kallaghe alisisitiza kwamba tusiwalaumu wanamichezo kwa kushindwa kwani kuna mataifa mengi yaliyokosa medali. Tafrija hiyo ilihudhuhuriwa na maofisa wote wa Ubalozi, wanahabari London na Balozi wa Rwanda Uingereza, mheshimiwa Ernest Rwamucyo.
Kitakwimu ni asili mia kumi tu ya washiriki 10,500 waliocheza michezo 26 (toka mataifa 204) wakapata medali. “Kuna mataifa tajiri kama Ujerumani, Australia na India ambayo hayakufanya vizuri na pia wenzetu Afrika mfano Kenya na Ethiopia ambao hawakuridhika au kufikia nafasi waliyozoea miaka iliyopita.”
Balozi aliitaja nchi ya Wafilipino (Philippines) yenye watu Milioni 93 ambayo ilikuwa na wachezaji 11 na haikuambulia kitu. Kidesturi toka 1936, Wafilipino wamekuwa wakishinda medali katika mchezo wa ngumi.“Lazima tujiulize maswali ili kufanikiwa mashindano yajayo na kujitayarisha ndiyo msingi. Vipaji vingi vipo Tanzania. Tujaribu kuangalia na kujiuliza wapi vilipo vianzio vya kuendeleza michezo yetu kutoka ngazi za chini maana uwezo wa kushinda tunao. ”
Akipigiwa makofi balozi alimtaja mkimbiaji maarufu wa Uingereza mwenye asili ya Kisomali, Mohammed “Mo” Farah aliyefanya vibaya sana Olimpiki ya 2008, China. “Baada ya kushindwa kabisa Beijing, Mo Farah alijilaumu na kulia sana; ila hakuvunjika moyo; alirudi akajiandaa vizuri na matokeo yake mwaka huu kashinda medali mbili za dhahabu.”
Naye mkuu wa msafara Bwana Hassan Jarufu aliushukuru ubalozi wetu Uingereza kwa ukaribisho mzuri uliohakikisha kwamba wanamichezo wako sawa toka walipowasili hapa majuma mawili kabla ya Olimpiki. Aliwataja pia wasaidizi wenyeji wa Uingereza, Alison Cochrane, Steve Wiseall na Lesley Shayler aliyewahi kuitembelea Bongo na kuipenda sana.“Hawa wamekuwa wenyeji wetu wazuri sana,” alisema.Jarufu alifahamisha kwamba wanamichezo wetu shurti kupongezwa kwa kujitahidi kufanya shughuli hii bila ajira au kazi maalum.
“Kwa mfano wakimbiaji wa mbio za marathon wanatakiwa kiafya wakimbie mara nne tu kwa mwaka kusudi wawe tayari kwa mashindano makubwa, lakini kutokana na kukosa ajira au msaada wa kifedha wanalazimika kushindana mara nyingi zaidi ili waishi. Na si ajabu ukamsikia mmoja mmoja akilalamika kashindwa mashindano makubwa kama Olimpiki kutokana na majeruhi fulani mwilini.”
Katika michuano ya siku ya mwisho Jumapili wanariadha watatu, Faustin Mussa, Samson Ramadhan na Mohammed Msondiki Ikoki walishiriki mbio za marathon na hawakupata.
Picha na Urban Pulse wakishirikiana na Freddy Macha
0 Comments