Mshambuliaji wa Simba ,Haruna Moshi 'Boban' akimtokea beki wa Azam Said Moradi katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Kagame mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Na Clezencia Tryphone
HESABU za mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, kutaka kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa Kombe la Kagame tangu mwaka 2002, jana zilifutika baada ya mbio zao kuishia mikononi mwa Azam FC
.
Simba mabingwa mara sita wa michuano hiyo tangu kuasisiwa kwake mwaka 1974, jana walikumbana na kichapo cha mabao 3-1 katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo ya 39.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ilishuhudia Azam wakicheza soka ya uhakika hadi kuwafunika Simba tangu kipindi cha kwanza.
Licha ya kiwango cha Simba kuonekana kuimarika kiasi tofauti na mechi tatu zilizopita, lakini walijikuta wakizidiwa na vijana wa Hall, waliokuwa na kila sababu ya kushinda.
Simba walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kali langoni mwa Azam katika dakika ya 11, lakini shuti la Uhuru Seleman, lilidakwa na kipa Deogratius Munishi.
Dakika ya 14, Ramadhan Chombo alifumua shuti lakini likienda nje kabla ya Balou Kipre kutoka baada ya kuumia eneo la kifundo cha mguu.
Azam wakicheza soka ya kutulia zaidi na kufanya mashambulizi ya uhakika, walipata bao la kwanza dakika ya 18, likifungwa kwa kichwa na John Bocco ‘Adebayor’ akiitendea haki pasi ya Ibrahim Shikanda.
Pamoja na Simba kupambana vilivyo kusawazisha bao hilo, lakini hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Azam washindi wa pili katika Ligi Kuu ya Bara, walikuwa
mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Simba kusaka bao la kusawazisha huku Azam wakitaka kuongeza la pili, lakini alikuwa Adebayo kwa mara ya pili aliyewainua vitini wapenzi wa Azam baada ya kuifungia timu yake bao la pili.
Adebayor alifunga bao hilo dakika ya 46, akimalizia kazi nzuri ya Kipre Tchetche, hivyo kuwafanya Simba kuwa nyuma kwa mabao mawili huku uwanja ukirindima kwa shangwe na nderemo za mashabiki wa Azam FC wakipigwa tafu na wale wa Yanga.
Bao hilo liliwafanya Simba kuongeza wakijaribu kupanga mashambulizi ya uhakika huku mabeki wake wakiwa na kazi ya ziada kuwadhibiti Salum Aboubakar, Adebayor, Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha.
Juhudi binafsi za beki wa kushoto wa Simba, Shomari Kapombe, za kupanda kusaidia mashambulizi zilizaa matunda baada ya kuifungia bao timu yake katika dakika ya 53
kwa shuti kali ya mita 18 kutoka langoni.
Bao hilo liliwapa nguvu Simba wakiongeza presha ya mashambulizi, lakini Azam nao wakicheza kiwango cha kuvutia na dakika ya 73, Adebayor alirejea kwa mara nyingine kwenye lango la Simba na kumpeleka Kaseja mara ya tatu nyavuni.
Adebayor, nyota aliyekuwa ameisusa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, akikerwa na shutuma za mashabiki kabla ya kurejeshwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
alifunga bao hilo kwa shuti kali la nje ya mita 18.
Baada ya Adebayor kufunga bao hilo, Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicolas Musonye, alihamaki kwa kujishika kichwa huku akijisemea ‘My God’! Akimaanisha Mungu Wangu.
Licha ya Simba kupambana vilivyo kusaka mabao ya kusawazisha, Azam walikuwa imara wakifanya mashambulizi na kukabiliana na mashambulizi, hivyo hadi filimbi ya mwisho, Azam walikuwa wababe kwa mabao 3-1.
Kwa ushindi huo, Azam inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake Juni 24, 2007, itakutana na AS Vita ya DR Congo katika mechi ya nusu fainali itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Wakati Azam wakiwafunga Simba, AS Vita waliwang’oa mabingwa wa Burundi, Atletico, kwa kuwatungua mabao 2-1 katika mechi ya mapema jana iliyochezwa pia kwenye uwanja huo wa Taifa.
AS Vita walianza kupata bao dakika ya saba, likifungwa na Etekiama Teddy kabla ya Piere Kwizera kuisawazishia Atletico kipindi cha pili, lakini Vita wakaongeza la pili dakika ya 90.
SIMBA: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Lino Musombo, Jonas Mkude, Salum Kinje/Mussa Mude, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’ na Uhuru Selemani/ Kiggy Makassy.
AZAM: Deo Munish, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Saidi Moradi, Aggrey Morris, Balou Kipre/ George Odhiambo, Salum Aboubakar, John Bocco ‘Adebayor,’ Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha/Jabir Azizi.
0 Comments