MBUNGE wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM),jana ameilipua Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, akidai imeshindwa kusimamia michezo, hivyo ni bora ikiwa idara ndani ya wizara nyingine kuliko kutumia fedha wanazotengewa kila mwaka kwa matumizi yao binafsi.
Azzan alisema kuwa uzembe huo umeifanya wizara kushindwa kukamilisha mchakato wa kuandaa sera ya michezo ya taifa tangu mwaka 2006, hivyo kuwaponda watendaji wakuu kuwa wameshindwa kuweka kipaumbele katika michezo.
Katika hatua hiyo, mbunge huyo alifichua kuwa Kamati ya Olimpiki Tanzania imeshindwa kuwalipa posho ya siku kumi wachezi wake wanaoshiriki michezo hiyo jijini London, hivyo amedai ni miujiza tu kwatimu hiyo kurudi na medali.
“Mheshimiwa Spika, zimekuwa zikitolewa fedha nyingi kwa TOC kutoka Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), lakini haijulikani zinafanya nini, zinawanufaisha kina nani badala yake hata wakati mwingine wachezaji wanashindwa kulipwa,” alisema.
Alihoji pia kitendo cha TOC kuishia kujenga kituo cha michezo licha ya kupewa fedha akidai kuwa wadau wa michezo wameanza kutilia shaka uongozi wa kamati hiyo nchini, huku kukiwa na taarifa kuwa Katibu Mkuu wake, Filbert Bayi, ndiye amekwamisha ujenzi huo kwa makusudi kwa vile kambi ya wachezaji imekuwa akiiweka kwenye shule yake.
Azzan pia alilishukia Shirikisho la Soka Tanzania (TTF), akisema katika sakata
la aibu lililotokea mbele ya Rais Jakaya Kikwete kwenye michuano ya Afrika Mashariki ya Kati katika Uwanja wa Taifa kwa taa kuzimika wakati wa kukabidhi zawadi na nyimbo za taifa kushindikana kuimbwa mwaka jana, ni mtu mmoja tu amechukuliwa hatua.
“TFF ilimtosa aliyekuwa Afisa Habari, Florian Kaijage, katika sakata lile la aibu kwenye michuano ya mwaka jana kwa kumwachisha kazi lakini meneja wa uwaja huo yeye mpaka sasa ameachwa badala yake alisimamishwa kwa mwezi mmoja,” alisema Azzan.
0 Comments