Mkoa wa Mwanza hatimaye nao umepata vipaji vitakavyoiwakilisha katika tamasha la washindi wa tunzo za muziki za Kilimanjaro, litakalofanyika katika uwanja wa Kirumba jijini humo, Mei 5 mwaka huu.
Tofauti na mkoa wa Dodoma, ambapo jumla ya vijana wenye vipaji 241 walijitokeza, Mwanza kulikuwa na idadi kubwa ya vijana waliojitokeza, mara mbili ya Dodoma lakini cha kushangaza, wengi wao walikuwa wakiimba vitu vinavyofanana au kuwa na aina moja ya uimbaji jambo ambalo liliwachanganya sana majaji.
Kwa mujibu wa wasimamizi wa mchakato huo, kampuni ya Flontline Novelli, jumla ya wasanii 506 walijitokeza, na kusababisha kufanyika kwa mzunguko mmoja tu kwa siku ya kwanza, na mizunguko mingine kufanyika siku inayofuata.
Katika mzunguko wa kwanza, ambao ulifanyika jumapili jumla ya washiriki 57 walipatikana ambao waliingia katika raundi pili na baada ya mchujo walipatikana 16 na kisha watano na kisha watatu.
Watatu waliopatikana ni bertha dennis ambaye alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kugeuza sauti na kuimba nyimbo mbali mbali za kunakili na utunzi wake, mwingine akawa Christian Joachim na wa tatu akawa ni marcus Antwan.
Mchakato mzima ulifanyika katika ukumbi wa Villa Park ambapo kama kawaida wiki hii tena, majaji Joseph Haule, Juma Nature, Henry Mdimu na Queen darleen.
Wakiongelea kwa nyakati tofauti Majaji hao wameutaja mkoa wa Mwanza kuwa mkoa mgumu kuliko mkoa wa Dodoma ambao walianza nao, ulikuwa na watu wengi wanaofanania kwenye kazi zao.
"Wako kama wanaigana hivi na tunakiri kwamba wazuri walikuwa wengi lakini tulilazimika kuwaondoa kwenye mashindano kutokana na ukweli kwamba tulikuwa tunatafuta zaidi ya kipaji", Queen Darleen alisema wakati akielezea mchakato mzima wa mkoa wa Mwanza.
Washindi watatu wa Mwanza watapata nafasi ya kurekodi wimbno mmoja kila mmoja na kisha kurekodi mwingine wa pamoja, nyimbo ambazo wataziimba kwenye tamasha la Jumamosi hii inayokuja, ndani ya viwanja vya Kirumba.
Washindi hao watachujwa na nguvu ya wananchi siku ya Jumamosi ambapo mmoja kati yao atapata nafasi ya kushiriki katika tamasha kubwa litakalofanyika jijini Dar es salaam, na pia atapata nafasi ya kurekodi wimbo mmoja zaidi ya ule ambao ataurekodi wiki hii kabla ya tamasha.
0 Comments