ABAMTO AtTAMBA NA SINGO YA WEMBE,AOTA KUWA NYOTA BARANI AFRIKA


 Msanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya, Abamto, amedhamiria kulikamata soko la muziki wa vijana ukanda wa Afrika Mashariki na hatimaye Afrika nzima kwa kufanya kazi za kiwango cha kimataifa ili kuleta mapinduzi ya kweli ya muziki huo kimafanikio.


Abamto ambaye jina lake halisi ni Abdallah Ali Mtonyi, amepasha kuwa, siku zote kabla na baada ya kuanza kujihusisha na kazi ya muziki kama mtunzi na muimbaji, ndoto yake kubwa ni kuwa staa wa bara la Afrika na panapo majaaliwa awike kidunia.


"Nimeanza kazi ya muziki kwa wimbo wangu wa WEMBE ambao pamoja na juhudi zangu na watayarishaji, namshukuru Mungu kwa kujaalia mapokezi mazuri kwa kazi hiyo. Ni mwanzo tu wa safari yangu ndefu ya sanaa ambayo natamani hatima yake iwe nimekuwa nyota wa kimataifa kwa bara la Afrika kama akina Baaba Maal, Youssou N'Dour, Mori Kante, Femi Kuti, 2Face Idibia na wengine kadhaa," akasema.


Akizungumzia wimbo wa Wembe, Abamto anayefanya kazi chini ya zao la kampuni ya Kiumbe (Kiumbe Productions), amesema kuwa, pamoja nao bado ana tungo nyingi ambazo amezifanyia muziki kwa ubora wa kiwango cha juu sanjari na mchanganyiko wa mitindo ya house na techno ambayo imeongeza utamu wake.


"Nimerekodi studio za Kiumbe Productions chini ya mtayarishaji wa ukweli Masoud Composer na Udy na hivi sasa niko mbioni kufanya video na kampuni hii hii (Kiumbe). Najiamini kwa kutawala jukwaa (kudansi) sambamba na madansa wangu wakali wa ku-swing na ku-shake," akanena Abamto akitoa tambo.


Alipoulizwa ni msanii gani anayemzimia kwa sasa hapa nchini, Abamto alimtaja nyota mwingine aliye chini ya lebo hiyo, Matonya, huku akimmwagia sifa Meneja wa kampuni hiyo Hussein Makatta na Bi Amina na wanafamilia wote wa Kiumbe Productions.

Post a Comment

0 Comments