Na Mwandishi Wetu
MWIMBAJI nguli kutoka Kenya, Solomon Mukubwa, anatarajia kuzindua albamu yake mpya ya nne ya Utukufu wa Mungu katika tamasha la muziki wa Injili la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ambaye ni Mkurugenzi wa Msama Promotions, alisema Dar es Salaam jana kuwa Mukubwa ameahidi kufanya mambo makubwa atakapotumbuiza.
Msama alisema mwimbaji huyo wa nyimbo za kumsifu Mungu mwenye ulemavu wa mkono mmoja, hivi sasa anatamba na albamu hiyo anayoamini itamng'arisha katika tamasha hilo.
Kabla ya Utukufu wa Mungu, Mukubwa amewahi kutamba na albamu ya Usikate Tamaa yenye nyimbo za Usikate Tamaa, Mungu Wangu Nitetee, Niko na Yesu, Mke Si Nguo, Moyo Tukuza Bwana, Chunga Ahadi Yako na Yesu Jina Zuri.
Mukubwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anayeishi Kenya, pia amewahi kutoa albamu mbili ambazo ni Sijaona Rafiki na Mungu Mwenye Nguvu.
Sijaona Rafiki Kama Yesu ambayo ni albamu yake ya kwanza ina nyimbo za Uwe Nami Bwana, Sijaona Rafiki Kama Yesu, Nitayainua Macho, Matendo ya Mungu, Bwana Wastahili na Yesu Kimbilio.
Albamu yake ya pili ya Mungu Mwenye Nguvu ina nyimbo za Mungu Mwenye Nguvu, Mkono wa Bwana, Mfalme wa Amani, Siku Moja, Tabia Ina Dawa na Roho Yangu Ikuimbie.
SOLOMON MUKUBWA
Mbali na Mukubwa, wengine waliothibitisha kushiriki tamasha hilo litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Anastazia Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti Faraja Ntaboba, Ephraim Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival.
Msama alisema baada ya waimbaji hao kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu.
Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.
0 Comments