Pichani kutoka kushoto ni kikosi cha bendi ya Kalunde waimbaji Mwapwani, Debora Nyange, Rais wa bendi Deo Mwanambilimbi na Sarafina Mshindo
Bendi ya muziki wa dansi ya Kalunde 'The Best' chini ya uongozi hodari wa Bob Rudala na Captain Deo Mwanambilimbi, imeongeza ratiba yake ya maonesho kwa kuanzisha shoo mpya ya kila siku za Jumapili ambapo itakuwa ikitumbuiza kwenye ukumbi wa Chichi Hotel uliopo Kinondoni B, jijini Dar es Salaam huku Sarafina Mshindo, Mwapwani Yahya na Deborah Nyangi wakitarajiwa kuwa kivutio kikubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, kiongozi wa bendi hiyo, Bob Rudala amesema kuwa, wameamua kupanua wigo wa shoo zao ili kuwapa burudani mamia ya maelfu ya washabiki wake ambao wapo kila kona ya jiji ambapo kwa kuanzia wameweka kambi yao ukumbi wa maraha wa hoteli ya kisasa ya Chichi iliyopo Kinondoni B kandoni mwa barabara ya Kawawa.
"Tulianza na kumbi kama Rainbow, Giraffe Ocean View, Cine Club, Peacock na kwingineko kuwafuata washabiki wetu ambao baadhi walishindwa kusafiri toka eneo moja kwenda jingine, sasa tumeamua kuwafuata wakazi wa Kinondoni waje kushuhudia muziki wetu ulivyo bora na ladha murua na kila atakayefika atabaki na kitu bora cha kusimulia popote aendako," akasema Rudala huku Captain Deo akiitikia kwa kichwa.
Rudala alitaja ratiba zingine za bendi hiyo kuwa kila siku za Ijumaa bendi yake hufanya shoo za kukata na mundu pale ukumbi wa TRINITY maeneo ya Oysterbay huku kila siku za Jumamosi wakimwaga burudani maeneo ya Kunduchi ndani ya ukumbi wa Kunduchi Beach Hotel. sanjari na hayo, Rudala aliahidi kuwa wanazifanyia kazi nyimbo zao mpya ambazo wakati wowote zitawekwa hewani.
0 Comments