MHARIRI MTENDAJI WA KAMPUNI YA FREE MEDIA ABSALOM KIBANDA ALIPOPANDISHWA KIZIMBANI

 Kushoto  ni Naibu Mhariri wa Kampuni ya Free Media wanaochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari Ansbert Ngurumo na Mhariri Mtendaji wa Kampuni hiyo Absalom Kibanda mara baada ya kutoka Mahakamani ambako alisomewa shitaka la tuhuma za uchochezi.
                                                        (PICHA ZOTE NA FRANCIS DANDE)  
 Kutoka kushoto ni Mhariri wa Michezo wa Gazeti la Tanzania Daima Tulo Chambo, mwandishi Shaban Matutu na Mchora  Vibonzo Said Michael wakifurahia jambo na Mhariri wao.  
 Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media  inayochapisha Magazeti ya Tanzania Daima  na Sayari , Absalom Kibanda (Kulia), akiongozana  na Mawakili wake, Juvenalis Ngowi (Kati) na Deo Ringia, wakati akitoka katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  Jijini Dar es Salaam jana,Desemba 20, baada ya kusomewa shitaka  la uchochezi. 
 Kulia ni Ofisa Usambazaji wa Kampuni ya Free Media Marcus Mtinga na Adam Mwenge wa Idara ya Matangazo
 Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya New Habari  Corporation Hussein Bashe, Absalom, Mkurugenzi Kampuni ya MwanaHalisi Said Kubenea na Wakili Deo Ringia.  
 Katibu wa Jukwaa la Wahariri Nevile Meena akimkumbatia Kibanda mara baada ya kupata dhamana.

TAARIFA YA BODI YA JUKWAA LA WAHARIRI (TEFF) KWA VYOMBO VYA HABARI  KUHUSU KUHOJIWA  KWA ABSALOM KIBANDA
UTANGULIZI
1. Ijumaa iliyopita, Mhariri Mtendaji wa Free Media Ltd, wazalishaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda alishikiliwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini.
2. Kiini cha tukio hili ni makala iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Novemba 30, 2011 ikiwa na kichwa kisemacho "Waraka maalum kwa askari wote".

3. Mwandishi wa makala hiyo, Samson Mwigamba ambaye tayari amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi analalamikia hulka ya polisi wa chini kutii amri hata kama amri hizo zina madhara kwa nchi na kwa mtizamo wake anasema hali hiyo inaweza kuifikisha nchi pabaya siku zijazo.

                                     UTENDAJI WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI
4. Umekuwa ni utamaduni kwa Msajili wa Magazeti ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) kuchukua hatua za kuvibana vyombo vya habari, hususan magazeti ambayo yamekuwa yakionekana kukiuka sheria za nchi katika uandishi wake.

5. Chini ya utaratibu huu ambao hata hivyo umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa habari, Maelezo humwandikia barua Mhariri husika kuhusu kosa linalodaiwa kufanywa katika gazeti lake, na kutaka atoe maelezo au afike katika ofisi hizo kwa ajili ya kuhojiwa.

6. Kupitia Maelezo, hatua mbalimbali zimechukuliwa na pande husika ikiwa ni pamoja na magazeti kupewa barua za onyo, kupewa fursa ya kusahihisha taarifa husika na katika matukio machache yasiyopendeza baadhi yamewahi kufungiwa na mengine kufutwa kabisa.

. Licha ya kasoro zake, jambo la msingi ni kwamba utaratibu wa Msajili wa Magazeti walau umekuwa ukitoa fursa watendaji wa magazeti yanayolalamikiwa kutoa maelezo ya upande wa pili lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba Uhuru wa Habari hauminywi kiasi cha kuukosesha umma taarifa muhimu za nchi na mambo yanayofanyika nchini.
                                                              KUKAMATWA KWA KIBANDA
Jukwaa la Wahariri limefuatilia kwa karibu sana tangu kukamatwa kwa Kibanda na mtindo uliotumiwa na Polisi katika kushughulikia suala hilo na kubaini yafuatayo:

8. Kwanza Makala ambayo ni chimbuko la kukamatwa kwa Mwigamba na baadaye Kibanda haikuwahi kulalamikiwa na Ofisi ya Msajili wa Magazeti kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa taarifa nyingine nyingi, si kwa gazeti la Tanzania Daima tu, bali hata kwa magazeti mengine.

9. Kwa maana hiyo hakuna barua yoyote kutoka Maelezo ambayo iliwasilishwa Tanzania Daima ikimtaka Mhariri Mtendaji kutoa maelezo ya kimaandishi au kufika kwa msajili kujibu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ama sheria katika makala hiyo ya Novemba 30, 2011.

10. Hakuna taarifa zozote za mtiririko wa kimatukio katika Idara ya Habari (Maelezo) au kwingineko Serikalini ambazo zinabainisha iwapo kulikuwa na onyo lolote kwa Tanzania Daima kuhusu mwenendo wake au kuhusu makala za Samson Mwigamba.

                                             MTIZAMO NA MSIMAMO WA TEF
11.Kutokana na hali hiyo, TEF inaona kwamba kuna msukumo usio wa kawaida nyuma ya hatua ya Polisi ya kumhoji Kibanda na kwamba mwelekeo ni kuminya uhuru wa Habari na Uhuru wa kujieleza ambao umetolwa chini ya misingi ya Katiba ya nchi.

12. Msukumo huu unatokana na kuibuka ghafla kwa vyombo vya dola na zamu hii Polisi wakitumia muda mrefu katika kile walichokiita kuwa ni uchochezi, hivyo kuwafungulia wahusika KESI ZA JINAI.

13. Mashtaka haya dhidi ya Kibada na Mwigamba yanatushawishi kuamini taarifa zisizo rasmi juu ya kuwapo kwa mpango wa kuwashughulikia baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari ambao wamekuwa msitari wa mbele kukosoa waziwazi miendendo ya watawala.

14. Sisi tunasema hali hii haikubaliki kwani inalenga kurejesha demokrasia ya Taifa hili nyuma zaidi ya miaka 50 iliyopita, kwa kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kutoa na kupata habari.

15. Mwenendo wa aina hii wa kuamu kuwashati wahariri kwa makosa ya jinai ni hatari kwa mustakabali wa nchi yetu, hasa pale vyombo vya dola vinapotumika kwa mtindo ambao umetumiwa kuwashughulikia Kibada na Mwigamba.

16. Ikumbukwe kwamba dhamira ya kupambana na wakosoaji wa utendaji Serikalini siyo tu kwamba inaathiri dhana nzima ya utawala bora wa nchi, bali inaliweka Taifa katika hatari ya kutumbukia katika uovu uliokithiri hasa pale wenye dhamana watakapofanya wapendavyo kwa kuwa tu vyombo vya habari vitakuwa vibezibwa midomo.

17. Kwa kuwa hii inaonekana kuwa dhamira rasmi ya Serikali kutumia dola kudhibiti uhuru wa habari, tunatoa mwito kwa watawala wetu kutafakari upya na ikiwezekana kuachana kabisa na dhamira hiyo.
  NEVILLE MEENA,
  KATIBU MKUU – TEF
  KWA NIABA YA BODI YA JUKWAA LA WAHARIRI

 Wahariri wakijadiliana  jambo nje ya Mahakama ya Kisutu jana Des.20
 Kushoto ni Mhariri Jabir Idrissa  na Kibanda  mara baada ya kupata dhamana.
 Wanahabari wakichukua maelezo mafupi nje ya Mahakama  kutoka kwa Wakili wa Nyaronyo Kicheere .
 Hapa wakati akishuka katika gari lililompeleka Mahakamani.hapo.
 Baadhi ya wanahabari wakiwa katika varanda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Desemba 20 ambapo wakisubiri kuingia mahakamani kusikiliza kesi hiyo

Na Mwandishi Wetu.
MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Free Media inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda(45) jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na tuhuma za uchochezi.

Kibanda ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, jana alisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Stewart Sanga na kukana tuhuma hizo.

Mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Mwandishi wa safu maalumu wa gazeti hili, Samson Mwigamba, ambaye kwa mara ya kwanza alisomewa mashitaka hayo, Desemba 8 mwaka huu.

Akimsomea mashitaka hayo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa Kibanda na Mwigamba wanakabiliwa na mashitaka ya kuandika makala ya uchochezi inayowashawishi askari Polisi, askari Magereza na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuacha kuitii mamlaka iliyopo.

Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3:37 asubuhi akiongozwa na makachero wa Jeshi la Polisi, kisha kupelekwa chumba cha mahabusu wakati akisubiri kusomewa mashitaka hayo.

Wakati Kibanda akiwa mahabusu, nje ya mahakama waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini walifurika mahakamani hapo wakisubiri kusomwa kwa kesi hiyo.

Ilipotimu majira ya saa 11.13 asubuhi, Kibanda alitolewa mahabusu na kupelekwa chumba cha mahakama huku akiambatana na jopo la mawakili wake wanne, ambao ni Juvenalius Ngowi, Nyaronyo Kicheere, Isaya Matambo na Deogratius Ringia tayari kusikiliza mashtaka yanayomkabili, ambapo jopo hilo linaongozwa na Ringia.

Mbele ya Hakimu Sanga, Wakili Kaganda alitaja namba ya kesi kuwa ni 289/2011 na kuanza kumsomea mshtakiwa kesi yake kuwa ni kuruhusu gazeti lake la Novemba 30 toleo namba 2553 kuchapisha waraka uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka Maalum kwa Askari wote,” ulioandikwa na mshtakiwa mshitakiwa wa awali Mwigamba katika safu yake ijulikanayo kwa jina la ‘Kalamu ya Mwigamba.’

Wakili Kaganda alisema kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 46(b), 55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Baada ya kusomwa shtaka hilo na Wakili Kaganda, Hakimu Sanga alimuuliza mtuhumiwa kama anakubaliana na kosa hilo ambapo mtuhumiwa alikana kosa na hakimu kutoa masharti ya dhamana kuwa ni lazima wadhamini wawe wawili na wanaoaminika.

Pia alisema wadhamini hao lazima wasaini bondi ya sh milioni tano na mmoja kati yao awasilishe hati ya mali isiyohamishika, huku mshitakiwa akitakiwa kukabidhi hati yake ya kusafiria.

Kufuatia masharti hayo walijitokeza wadhamini wawili ambao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Publishers inayochapisha gazeti la Mwanahalisi Saed Kubenea na Ofisa wa Benki ya Posta Tanzania Ahobokile Mwanjoka ambao kwa pamoja walisaini bondi ya sh milioni tano na kuacha hati ya mali isiyohamishika mahakamani hapo.

Baada ya kukamilka kwa taratibu zote za dhamana mtuhumiwa aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kurejea tena katika mahakama hiyo Januari 19, 2012 kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo.

Desemba 16 mwaka huu Kibanda alijisalimisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, ambako alihojiwa kwa saa zaidi ya tatu na kuachiwa kwa dhamana ya sh milioni tano, iliyotolewa na Kubenea ambapo alitakiwa kurejea Polisi Desemba 19 jambo alilolitekeleza na kutakiwa kurudi jana ambapo ndipo walipomfikisha mahakamani.

Post a Comment

0 Comments