Kocha wa Timu ya Taifa Chad, Mohammed Oumar Yaya mwenye fulana nyekundu, Kocha Mkuu wa Taifa Stars Jan Poulsen, Ofisa Masoko wa kampuni ya Bia Serengeti na Meneja wa Bia Serengeti Allan Chonjo.
KOCHA wa timu ta Taifa ya Chad Mohamed Oumar Yaya amesema Watanzania wasibweteke na ushindi walioupata 2-1walipocheza kwao mwishoni mwa wiki N’djamena, nchini Chad.
Yaya aliyasema hayo leo wakati makocha wa timu hizo mbili walipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu kuelekea mechi hiyo muhimu itakayochezwa kesho katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo aliongeza kwa kusema kuwa jambo kubwa lililosababisha Chad ifungwe na Taifa Stars nyumbani kwao ni kwa sababu walicheza na timu ya watu ambao hawakuwa wakiwafahamu.
“Tumeona wapi tupokosea hivyo tumekuja na mbinu zetu na tutazionyesha kesho ambapo lolote linaweza kutokea” alisema Yaya.
Wakati huohuo Yaya amemwagia sifa timu ya Taifa Stars kwa kuwa na Kipa mahiri na wakutumainiwa ambaye ni Juma Kaseja ‘Tanzania One’ kwamba anastahili sifa zote za kuitwa kipa bora.
“Kipa huyu ni mzuri sana lakini katika mechi ya leo huenda mambo yakawa tofauti na ilivyokuwa N’djamena Chad, japo kule tulishindwa lakini sisi tumekuja hapa kwa lengo la kusonga mbele hivyo sina budi kusema timu bora ndiyo itakayoshinda katika mechi hii na tutashinda” alisema.
“Kwaniaba ya timu yangu nachukua fursa hii kuwashukuru Watanzania na kuwaambia kwamba tumefurahi kwa kupata mapokezi mazuri na hata kwa wale mashabiki ambao wamekuja kuangalia mazoezi na kutushangilia nasema asante sana” alisema Yaya.
Ulipofika wakati wa kuzungumza Kocha wa Taifa Stars Jan Poulsen aliongeza kwa kusema kwamba wachezaji wa timu ya Chad siyo wakuchezea ni wachezaji wenye mbinu, stamina, wanamiili mikubwa hivyo inahitajika nguvu ya ziada na kiada katika kuendeleza ushindi.
“Hii ni mechi muhimu na ngumu sana kwetu licha ya kuwa tulipata ushindi nchini Chad, lakini nimewaona ni timu ngumu, wachezaji wanajituma ipasavyo wawapo uwanjani ,wanajua namna ya kupeana pasi na mpira wanauweza, wanastamina ya kutosha hivyo tusiwabeze” alisema Poulsen.
Naye Kocha Msaidizi wa Taifa Stars Sylvester Mash, akizungumza kabla ya mkutano kuanza alisisitiza kwamba mechi ya leo itakuwa ngumu kwani wachezaji wa Chad wamekamilika hivyo tusiwabeze kwa kuwa wana sifa zote za kuitwa wachezaji soka wanaujua mpira, wanastamina , wanamiili mikubwa hivyo Taifa Stars inabidi itumie nguvu ya ziada kuweza kushinda .
Wakati huohuo Nahodha wa Taifa Stars Henry Joseph alisema yeye hawezi kusema maneno mengi hivyo mashabiki wa soka wasubiri dakika 90 ndiye mwamuzi lakini huku akisisitiza kwamba watarajie mambo mazuri.
Kama Taifa Stars itaweza kuibuka washindi katika mechi ya leo italazimika kukutana na mtihani mwingine mkubwa katika hatua ya makundi ambapo itapambana na timu za Ivory Coast , Morocco na Gambia ikiwa ni katika kusaka kufuzu hatua ya makundi kwa ajili ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014.
Ofisa Masoko wa Kampuni ya Bia Serengeti (SBL), Ephraim Mafuru ambao ndiyo wadhamini wakuu wa Taifa Stars kwa kupitia bia yao ya Serengeti aliongeza kwa kusema kuwa kwa niaba ya Kampuni hiyo anatoa shukran za dhati kwa Watanzania wote walionyesha mshikamano wao kuelekea safari ya Brazil.
“Nachukua fursa hii kuwaalika mashabiki wa mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi na kuwa pamoja tutashinda , SBL tuko pamoja katika kuiwezesha Taifa Satrs kwenda Brazil” alisema Mafuru.
0 Comments