WAKATI mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete, akiwa bubu kuizungumzia adhabu yake ya kusimamishwa kwa mwezi mmoja, baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamepinga nyota huyo kupewa adhabu hiyo.
Uongozi wa Yanga, juzi ulitangaza kumsimamisha kwa mwezi mmoja mchezaji huyo kwa madai ya utovu wa nidhaumu aliyouonyesha wakati wa mazoezi ya timu hiyo hivi karibuni mbele ya kocha wake Mganda, Sam Timbe, kwenye uwanja wao wa Kaunda.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwa njia ya simu leo Tegete alisema kuwa hivi sasa hawezi kuzungumzia tukio, hadi hapo atakapokuwa sawa.
“Sitaweza kuzungumza chochote juu ya hilo, labda siku nyingine endapo nitakuwa sawa, ila kwa sasa siwezi sema chochote,” aliongea mchezaji huyo na kukata simu.
Kwa upande wao, baadhi ya wanachama wa Yanga, walitoa maoni yao juu ya suala hilo la kumfungia nyota huyo wakati kwa sasa inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu bara, wakidai ilitakiwa kamati ya ufundi kukaa na kujadili kwa kina suala hilo na sio kuchukua uamuzi wa haraka kama huo ambao ni tatizo kwa timu.
“Suala la kumchukulia Tegete maamuzi ya haraka ni kumvunjia heshima na ni maamuzi yasiyo ya busara, kwani Yanga ina taratibu zake, hivyo kamati ya nidhamu ilitakiwa kukaa na wahusika wote wawili, ambao ni Tegete na Sam Timbe ili kuzungumzia suala hilo la utovu wa nidhamu ambalo linamkabili nyota huyo dhidi ya kocha, kabla hawajatoa adhabu hiyo,” alisema mwanachama Saidi Bakari.
Naye mwanachama Charles Shinyambala alisema kwa sasa klabu inakabiliwa na mambo mengi, kuanzia kwenye suala la migogoro kwa viongozi na kuburuza mkia katika ligi, hivyo badala ya kamati kukaa kwanza na kulifanyia kazi suala hilo la Tegete, imetoa uamuzi wa moja kwa moja ambao hauna faida kwa timu na klabu kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kitendo hicho ni tatizo kubwa kwani kuna mechi ambazo atazikosa na mchango wake ni muhimu katika timu, hivyo kamati ilitakiwa kukaa kwanza kabla ya kutoa uamuzi.A
0 Comments