Na Bakari Kimwanga
SALAAM Aleikum mpenzi msomaji wa safu hii ya Fadhila za Ramadhani, ni matumaini yangu u-mzima na bukheri wa afya ukiwa unaendelea na swaumu yako ambapo leo ni Ramadhani 26, ikiwa ni Ijumaa ya mwisho katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani unaoelekea ukingoni.Kubwa ambalo hivi sasa kila mwislamu anajiandaa na sherehe ya Sikuu ya Idd El Fitri ambapo husherehekewa mara baada ya mfungo wa Ramadhani.Leo hii tunakumbushwa kwa kila aliyefunga mwezi wa Ramadhani na akawa anamiliki chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaatul Fitri, ambayo ni pishi ya tende, pishi ya ngano au pishi ya shayiri.
Maana ya Zakat –ui Fitri
Maana ya Zakat-ul-Fitr au Sadakaa l-Fitr ni ‘Sadaqa ya utakaso wa kufungua Saumu. Nacho ni kiwango fulani cha chakula kinachotolewa na Waislamu katika siku chache za mwisho wa Ramadhani au siku ya ‘Idd asubuhi, kabla ya kuswaliwa Swala ya Idd’.Na hii anatakiwa atoe kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile watoto wake, mke wake/wake zake na kuwapa maskini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.Kwa vipimo vya kisasa, pishi moja ya mbao iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kiasi cha kilo mbili.Zakaa hii ni wajibu kwa kila Mwislamu mdogo na mkubwa, mwanamume au mwanamke. Ibn ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:“Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amefaridhisha kwa kila mtu kutoa Zakaatul Fitri katika mwezi wa Ramadhani, pishi ya tende (au) pishi ya shaiyri, ikiwa yeye ni mtumwa au mtu aliye huru, mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislamu”.
[Al-Bukhaariy na Muslim].Hekima yake
Zakaatul Fitri ilifaridhishwa katika mwezi wa Shabaan Mwaka wa pili baada ya Hijra kwa ajili ya kumtwaharisha aliyefunga kutokana na makosa yoyote yale aliyotenda katika mwezi wa Ramadhani pale alipokuwa amefunga, kutokana na mazungumzo ya upuuzi au madhambi, na wakati huo huo Zakaah hiyo itawafaa maskini na wahitaji ili nao wapate kufurahi pamoja na Waislamu wenzao katika sikukuu. Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:
“Mtume (S.A.W) amefaridhisha Zakaatul Fitri kwa ajili ya kumtwaharisha aliyefunga kutokana na maneno ya upuuzi au madhambi madogo madogo na ili maskini nao wapate chakula. Atakayeitoa (Zakakaah hiyo) kabla ya Swalah (ya Idd) inakubaliwa Zakaah yake, ama atakayeitoa baada ya Swalah (ya Idd), itahesabiwa kama ni Sadaka ya kawaida.”
Abu Daawuud na Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy.
Nani mwenye kuitoa?Anayeitoa Zakaah hiyo ni mtu aliyefunga, anajitolea yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wanaomtegemea na anawatolea pia wote wale wanaomtegemea wakiwamo watumishi wake.Kiasi chake.Iliyowajibishwa katika Zakaatul Fitri ni pishi ya ngano au ya shayiri au ya tende, zabibu, mchele au ya mahindi na vinginevyo vilivyo na mfano huo katika vyakula.Imaam Abu Haniyfah peke yake ameeleza hata kutoa pesa zenye thamani hiyo badala ya kutoa nafaka kama kuna udhuru.
Wakati wa kuitoa
Maulamaa wengi wamekubaliana kuwa Zakaatul Fitri itolewe katika Ramadhani ya mwisho, lakini wamekhitalifiana juu ya wakati maalumu unaowajibika kuitoa.
Wapo waliosema kuwa wakati unaowajibika kuitoa ni pale jua la Ramadhani ya mwisho linapozama, na wengine wakasema kuwa wakati wake ni kuanzia baada ya kuingia alfajiri ya siku ya sikukuu.Kutokana na hitilafu hii tunapata faida ya kuwajibika kumtolea Zakaah hiyo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya sikukuu na baada ya jua kuzama, je, mtoto huyo anatolewa Zakaah?
Kwa wale wenye kufuata rai kuwa wakati wa kuitoa Zakaah hiyo ni pale jua la siku ya Ramadhaani ya mwisho kuzama, mtoto huyo hatolewi Zakaah kwa sababu amezaliwa baada ya kumalizika wakati wa kuwajibika, na kwa wenye kufuata rai ya pili, kwa sababu amezaliwa kabla ya wakati unaomwajibika.
Kuitanguliza kabla ya wakati wake
Maulamaa wengi wanakubali kuwa Zakaatul Fitri inaweza kutangulizwa na kutolewa kabla ya wakati wake kwa siku moja au mbili. Hadiyth iliyopokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) inasema;
“Mtume (S.A.W) ametuamrisha kuitoa Zakaatul Fitri kabla ya watu kutoka Msikitini (katika Swalah ya Idd),".Anasema Nafi’ (Radhiya Llaahu ‘anhu):“Ibn ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akiitoa kwa siku moja au siku mbili kabla ya Siku ya Sikukuu.”Ama zaidi ya hapo, Maulamaa wamekhitalifiana.Imaam Abu Haniyfah amesema: “Inaweza kutolewa wakati wowote ule katika mwezi wa Ramadhan.”Imaam Ash-Shaafi’iy amesema: “Inajuzu kuitoa (hata) katika siku za mwanzo za mwezi wa Ramadhaan.”Imaam Maalik amesema: “Inajuzu kutanguliza kwa siku moja au mbili kabla ya Sikukuu.”Lakini Maulamaa wote wamekubaliana kuwa haijuzu kuiahirisha na kuitoa Zakaatul fitri, hivyo ni vema wewe kama Mwislamu kutambua una wajibu wa kuitoa kama tunavyopata mafundisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wetu Muhamad (S.A.W).Maoni:0688 247 327bkimwanga@yahoo.com.
LEMA AMTAKA MBOWE KUSIKILIZA USHAURI WA FAMILIA YAKE WA KUTOGOMBEA TENA
-
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amtaka
mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe kutogombea tena nafasi hiyo kama
alivyosh...
42 minutes ago
0 Comments